Mkurugenzi Mtendaji Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya Bw. Bernard Konga akisema jambo wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Baraza la Pili la Wafanyakazi wa Mfuko huo Jijini Dodoma.
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dkt Binilith Mahenge akisema jambo wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Baraza la Pili la Wafanyakazi wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya.
Na NHIF - Dodoma
Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya, Bw.
Bernard Konga amesema kuwa mikakati yote inayowekwa na Mfuko huo inazingatia
maslahi ya wanachama na wananchi kwa ujumla katika uimarishaji wa huduma za
matibabu nchini.
Hayo ameyasema mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dkt. Bilinith
Mahenge wakati wa ufunguzi wa Baraza la Wafanyakazi la Mfuko ambalo limeketi
leo kwa lengo la kujadili masuala mbalimbali yakiwemo ya uimarishaji wa huduma
na mikakati ya kuwafikia wananchi katika maeneo yote.
“Nikuhakikishie Mkuu wa Mkoa kuwa timu iliyoko hapa ya
Wajumbe wa Baraza itahakikisha inaweka mipango inayozingatia maslahi ya
wanachama wetu lakini pia utekelezaji wa azma ya Serikali ya kuhakikisha kila
mwananchi anakuwa kwenye utaratibu wa kupata matibabu kwa bima ya afya,”
alisema Bw. Konga.
Alisema kuwa mikakati iliyopo kwa sasa ni kuyafikia makundi
yote yakiwemo ya wakulima, wavuvi, wafugaji, wakwezi na makundi mengine na hili
litafanikiwa kupitia uanzishwaji wa vifurushi vipya ambavyo vina gharama nafuu
kwa kila mwananchi.
Mkurugenzi Mkuu alisema kuwa, Mfuko unatarajia kuzindua
rasmi mpango wa vifurushi vipya mwezi Machi mwaka huu ambavyo vimeandaliwa kwa
kuzingatia mahitaji halisi ya wananchi katika huduma za matibabu.
Akifungua baraza hilo, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dkt. Mahenge
alisisitiza juu ya uwekaji wa mikakati ya kuwafikia wananchi wa ngazi zote ili
kuwezesha kila mtanzania kuwa na uhakika wa kupata matibabu yenye wakati wowote
anapopatwa na maradhi.
Alitumia fursa hiyo pia kuupongeza Mfuko kwa jitihada mbalimbali
za uimarishaji wa huduma za matibabu nchini ikiwemo uwekezaji katika ujenzi wa Hospitali ya Benjamin Mkapa na
maeneo mengine ambayo Mfuko umekuwa na mchango mkubwa katika kuboresha
miundombinu.
“Wajumbe wa kikao hiki hakikisheni mnatumia muda wenu vizuri
kwa kuweka mikakati ambayo ni imara itakayoufanya Mfuko uhudumie watanzania
wote lakini pia vizazi na vizazi,” alisema Mkuu wa Mkoa.
Mwisho.
0 on: ""TUMEWEKA MBELE MASLAHI YA WANACHAMA WETU" - Mkurugenzi Mkuu NHIF"