Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile (kushoto) akisalimiana na Mwenyekiti wa IPP Dkt. Reginald Mengi (kulia) kwenye mkutano wa wadau wa afya Jijini Dar Es Salaam.
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto Dkt.
Faustine Ndugulile (kushoto) akisalimiana na wadau wa sekta ya afya.
Na Mwandishi Wetu - Dar Es Salaam.
Teknolojia ya Seli Shina (Sterm Cell) ambayo inatumia chembechembe za seli za
mwanadamu kutibu kiungo chochote katika mwili husika, inatajwa kuwa na uwezo
mkubwa wa kutibu magonjwa mpaka yasiyoambukiza yakiwemo saratani zote, utindio
wa ubongo, seli mundu, kisukari, ualbino na kupooza.
Akizungumza kwenye mkutano wa kwanza wa kimataifa wa
wataalamu wa tiba za magonjwa ya binadamu jijini Dar es Salaam jana, Mwenyekiti
wa IPP, Dk. Reginald Mengi, alibainisha tiba hiyo ya seli shina ina uwezo
mkubwa na tayari imethibitika duniani kumrudisha mtu aliyefika hatua ya uzee
kuwa kijana mwenye afya njema.
Dk. Mengi kupitia kampuni yake ya IPP - Utafiti, Teknolojia
na Ugunduzi, akishirikiana na wataalamu mbalimbali duniani, amesema ataanzisha
maabara hiyo jijini Dar es Salaam, ambapo hatua iliyofikiwa mpaka sasa ni
upatikanaji wa vibali kutoka serikalini.
Alisema kuanzishwa kwa maabara hiyo hakuna maana kwamba
anapingana na uumbaji wa Mungu kuwa ni lazima binadamu afe, lakini lengo ni
kuhakikisha wale wanaopitia maumivu na tabu kubwa kutokana na kukosa tiba ya
magonjwa yanayowasumbua yakiwemo yanayotokana na umri mkubwa wanapata tiba hapa
hapa nchini.
Akizungumza kuhusu hatua hiyo, Naibu Waziri wa Afya,
Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Faustine Ndugulile, alisema serikali
haina tatizo juu ya hilo, kwa sababu ni maendeleo makubwa kwenye sekta ya afya
nchini na kumtoa hofu Dk. Mengi kuwa vibali hivyo vitapatikana haraka.
Lakini pia alisema kuwa serikali imetumia nguvu kubwa
kuboresha sekta ya afya kwenye uboreshaji miundombinu na kuanzisha tiba mpya
ambazo awali hazikuwepo hapa nchini ikiwemo upandikizi wa figo, uongezaji wa
bajeti, upandikizi wa ini na ute wa mifupa 'Bone Marrow'.
Alisema tiba ya seli shina ni ya kisasa, ikiwa na uwezo
mkubwa wa kutibu mtu kutokana na seli zake mwenyewe lakini alitahadharisha kuwa
kwenye kila hatua ya tiba hiyo lazima maadili yazingatiwe na miiko ya kitabibu
kama zinavyoelekeza kanuni za kada hiyo kote duniani.
Dk. Ndugulile alisema serikali itaendelea kushirikiana na
sekta binafsi kwenye uboreshaji wa sekta ya afya ili kuhakikisha kunakuwa na
kasi kubwa ya maendeleo kwenye eneo hilo lililo uti wa mgongo wa maendeleo ya
sekta zingine zinazotengemea nguvu kazi ya binadamu kwenye ukuaji wake.
Kwa upande wake Dk. Michael Magoti ambaye ni Mratibu mipango
wa IPP Utafiti, Teknolojia na Uvumbuzi, alisema mkutano huo wa kwanza wa
kimataifa umejumuisha wadau wa tiba kutokana nchi za Marekani, Australia,
India, Thailand, Vietnam na Egypt.
Alisema pamoja na maabara ya utafiti, Dk. Mengi kupitia
kampuni yake ya IPP Utafiti, Teknolojia na Uvumbuzi ana mpango wa kuanzisha
kliniki ya tiba kwa watoto wenye utindio wa ubongo ambayo itasaidia sehemu
kubwa ya watoto wanaozaliwa na matatizo ya kiakili kwa kutumia matibabu ya seli
shina hapa nchini.
Naye Profesa Dk. Kampon Sriwatanakul, raia wa Thailand
ambaye pia ni mtaalamu mshauri wa teknolojia hiyo ya tiba kutoka IPP, alisema
amejitoa kuja Tanzania kumsaidia Dk. Mengi kufikia ndoto yake ya kuwafikia
mamilioni ya watu wenye shida za kiafya ambazo tayari wamekata tamaa ya kupona.
Alisema kupitia teknolojia ya tiba ya seli shina, wana uwezo
mkubwa wa kutibu magonjwa mengi sugu ambayo kwa tiba za kawaida imeaminika kuwa
hayawezekani kwenye hospitali nyingi kubwa zikiwemo zile za kimataifa
zisizotumia teknolojia hiyo ya kisasa ya tiba.
Katika mkutano huo, jumla ya mada tisa zinazohusiana na tiba
ya seli shina ziliwasilishwa na wataalamu waliobobea kwenye kada ya afya kutoka
nchi kadhaa za Ulaya, Marekani na Asia.
0 on: "TANZANIA MBIONI KUNUFAIKA NA TEKNLOLOJIA YA SELI SHINA"