Na WAMJW-DAR ES SALAAM
Wananchi wametakiwa kujiunga na mfuko wa Bima ya Afya ili
kuondokana na adha wanayoipata pale wanapopata maradhi kwa kushindwa kugharamia
matibabu na kusababisha madeni , umaskini na pengine kifo.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii,
Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu leo wakati alipohudhuria mkutano wa
wadau wa Bima ya Afya kwa wananchi walio katika Sekta zisizo Rasmi uliojumuisha
wadau kutoka nchi mbalimbali uliofanyika katika ukumbi wa Hoteli ya Serena
jijini Dar Es Salaam.
“Tukiangalia hivi sasa asilimia 67 ya Watanzania wanalipa
huduma za matibabu kwa kutoa hela mfukoni, maana yake ni kwamba Watanzania hawa
wanapata changamoto pale ambapo wanapata maradhi kwa kutopata huduma nzuri kwa
sababu hawana fedha lakini pia wanapata changamoto ya kuingia katika umaskini kwa
sababu ya kugharamia matibabu”. Amesema Waziri Ummy.
Waziri Ummy amesema Wizara ya Afya kwa kushirikiana na
Shirika la Afya Duniani (WHO) pamoja na Shirika la Kazi Duniani (ILO) imefanya
tathmini mbalimbali na kugundua watu wengi hawana uelewa wa masuala ya Bima ya
Afya lakini wana uwezo wa kulipa. Kufuatia hali hiyo Serikali imeamua kuboresha
mfuko wa afya wa jamii “CHF Iliyoboreshwa” kwa gharama nafuu kwa watu watano
kwa mwaka ili kuwawezesha wananchi wengi kujiunga na mfuko huo.
“Hivi sasa asilimia 67 ya wananchi hawana Bima ya Afya,
hivyo wanatumia fedha taslimu kupata huduma. Hii ni changamoto kwa wengi kwa
kuwa matibabu yana gharama kubwa na ugonjwa huja bila taarifa”. Amesema Waziri
Ummy.
Kufuatia hali hiyo, Waziri Ummy ameeleza dhamira ya Serikali
kukamilisha mchakato wa kupitisha Sheria ya Bima ya Afya kuwa ni lazima kwa
kila mtu kabla ya mwisho wa mwaka huu 2019. Lengo la Serikali ni kuhakikisha
kupitia utaratibu huu wananchi wengi hasa wa kipato cha chini wanapata huduma
nzuri za matibabu na pia kuepuka kuingia kwenye umaskini kwa sababu ya ugonjwa.
Kikao hicho cha siku mbili kimejumuisha wajumbe kutoka nchi
za Kenya, Congo, Ghana, Cameroon, Ethiopia, Ujerumani, Ufilipino, Chad, Zambia,
Afrika Kusini, Uswisi pamoja na wenyeji Tanzania.
0 on: "WANANCHI WATAKIWA KUJIUNGA NA MFUKO WA TAIFA WA BIMA YA AFYA"