Madaktari wakimfanyia upasuaji mgonjwa wa Vikope (trachoma)
ambaye alifikia hatua ya kuelekea upofu katika zahanati ya Bahi-Makulu wilaya
ya Bahi mkoani Dodoma.
|
NA WAMJW-DODOMA
Maambukizi ya ugonjwa wa vikope (Trachoma) yameonekana
kupungua kwa zaidi ya aslimia 75 katika maeneo mbalimbali nchini.
Hayo yamesemwa leo na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii,
Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu wakati wa uzinduzi wa mpango wa taifa wa
kudhibiti magonjwa yaliyokua hayapewi kipaumbele katika Ukumbi wa Hotel ya
Morena jijini Dodoma.
Waziri Ummy amesema ugonjwa wa Vikope unawapata watu wa
jamii ya kimasikini hasa wafugaji na pia jamii yenye changamoto ya upatikanaji
wa maji safi.
“Trachoma ni ugonjwa ambao kwa kiasi fulani unahusiana na
umaskini na unawapata watu wa jamii ya wafugaji lakini pia wakiwa na changamoto
ya upatikanaji wa maji”. Alisema Waziri Ummy.
Aidha, waziri Ummy amesema katika kipindi cha miaka mitano
serikali imekua ikishirikiana na serikali ya Uingereza kupitia taasisi ya UK
aid na Queen Elizabeth Diamond Jubilee Trust katika kuhakikisha wagonjwa wa Vikope
wanafikiwa na kupata huduma za matibabu pamoja na kufanyiwa upasuaji kwa wale
ambao wanakaribia kupata upofu.
Waziri Ummy amesema bado kuna changamoto ya maambukizi
katika wilaya nane ambazo ni Mpwapwa, Chemba, Kalambo, Songwe, Ngorongoro,
Longido, Kiteto, na Simanjiro.
Hata hivyo katika kipindi cha miaka mitano wagonjwa wa
Trachoma waliofanyiwa upasuaji wamepungua kutoka 160,000 mwaka 2010 hadi
wagonjwa 17,000 mpaka mwezi Oktoba 2018, ambapo inatajwa kuwa ni hatua kubwa
katika mafanikio ya kukabiliana na maambukizi ya ugonjwa huu.
Waziri Ummy amesema serikali iko katika hatua nzuri ya
kuhakikisha inatokomeza maambukizi mapya ya Trachoma kwa kuendelea kutoa dawa
katika wilaya nane zilizotajwa na kuwafanyia upasuaji wagonjwa ambao wamefikia
hatua ya kupata upofu.
Naye balozi wa Uingereza nchini Bi. Sarah Cooke amesema
serikali ya Uingereza kupitia taasisi ya Queen Elizabeth Diamond Jubilee Trust na
shirika la SightServers itaendelea kushirikiana na serikali ya Tanzania
kusaidia kutokomeza ugonjwa wa Trachoma nchini.
MWISHO
0 on: "MAAMBUKIZI YA UGONJWA TRACHOMA YAPUNGUA KWA ASILIMIA 75 NCHINI"