Na WAMJWW
KATIBU Mkuu Wizara ya Afya,Maendeleo ya
Jamii,Jinsia, Wazee na Watoto amewataka watoa huduma na mafunzo kuhusu lishe
bora yaanzie ngazi za shule ya msingi ili kuwajenga watoto kuzingatia mlo bora
katika kukuza afya za watanzania.
Hayo ameyasema leo jijini Dar es salaam wakati wa
uzinduzi wa vitini vya mafunzo juu ya lishe bora katika jamii yetu
vilivyoandaliwa na Kanda ya mashariki ya kati na kusini inayojihusisha na maswala ya afya (ECSA).
“Walimu wawe sehemu ya afua za kufundishia
wanafunzi juu ya lishe bora hasa kuanzia ngazi za shule ya msingi ili
kuwajengea mazoea watoto kupenda kula mlo ulio bora hata wanapokuwa majumbani
mwao” alisema Dkt. Ulisubisya.
Aidha Dkt. Ulisubisya amesema kuwa baadhi ya
watoto walio vijini na mijini wana utapia mlo kwa kukosa chakula kilicho bora
hivyo jamii inatakiwa izingatie lishe bora ili kuimarisha afya za watoto
nchini.
Mbali na hayo Dkt. Mpoki amesema kuwa wahudumu wa
afya ngazi ya jamii wawe kipaumbele katika kutoa elimu ya lishe bora ili kuweza
kujikinga na Unyafuzi, Kwashakoo na magonjwa yasiombukiza kama vile
Kisukari,shinikizo la damu ,magonjwa ya moyo yanayotokana na ulaji kupita
kiasi.
Kwa upande wake Meneja wa Magonjwa yasioambukiza ,Usalama wa Chakula na
lishe ECSA Bi. Rosemary Mwaisaka amesema kuwa wameamua kuandaa vitini na vitita vya kufundishia lishe bora
ili kuweza kutoa elimu bora kwa watendaji na wahudumu ngazi ya jamii ili
kufikisha elimu hiyo kwa walengwa.
“Tumeamua kuandaa vitini hivi ili viweze kutoa
elimu bora kwa watendaji na wahudumu ngazi ya jamii ili kuweza kuwafundisha
wanajamii juu ya umuhimu wa kula mlo bora na vitatumika Kenya,Uganda na
Tanzania” alisema Bi. Mwaisaka.
Mbali na hayo Mshiriki wa Mafunzo ya Lishe bora
kutoka ECSA ambae pia ni Mtoa huduma Bi.
Evelyne Minja amesema kuwa mafunzo hayo yamewasaidia kutoa huduma katika jamii
kuhusu mlo bora hasa kwa watoto vijijini na mijini.
“Mafunzo haya yametufanya tujue jinsi ya
kuwahudumia na kutoa ushauri juu ya mlo bora hasa kwa watoto wenye viashiria
vya utapia mlo kwa kuwapima na kuwapangia vyakula vinavyostahili” alisema Bi.
Minja.
0 on: "DKT MPOKI ASISITIZA MAFUNZO YA LISHE BORA YAANZIE SHULE ZA MSINGI."