Mratibu wa Taifa wa mradi wa kupambana na usugu wa vimelea katika Shirika la chakula na kilimo duniani (FAO) Dkt. Bachana Rubegwa (aliesimama) akieleza maudhui ya semina hiyo niliyofanyika mapema leo katika ofisi za FAO.
Mwakilishi Mkuu wa mradi wa kupambana na usugu wa vimelea (FAO) Dkt.
Raphael Sallu akiwasilisha mchango wake wakati wa seminar na Waandishi
wa habari kuhusu matumizi bora ya antibiotic, ilofanyika katika ofisi za
FAO jijini Dar es salaam.
Mwakilishi wa Shirika la Afya Duniani (WHO) upande wa kupambana na usugu wa vimelea vya ugonjwa Bi Rose Shija akiwasilisha mchango mbele ya wadau wa habari, pembeni yake ni Afisa Habari wa Wizara ya Afya Catherine Sungura.
Mmoja ya wadau wa Habari ambae pia ni mmiliki wa Blog ya Full Shangwe akitoa mchango mbele ya wadau wenzie wa habari na wawakilishi wa Mashirika ya kimataifa katika Semina ya kuhamasisha matumizi bora ya antibiotic.
NA WAMJW-DAR ES SALAAM.
WATANZANIA wanatakiwa kwenda vituo vya kutolea
huduma za afya kupata vipimo kutoka kwa wataalam kabla ya kutumia dawa kwa
mazoea ili kuepuka usugu wa vimelea vya wagonjwa kwenye miili yao na
kusababisha vifo vya mara kwa mara.
Hayo yamezungumzwa na Mwakilishi wa Mkuu wa Mradi
wa kupambana na usugu wa vimelea kutoka Shirika la Chakula na Kilimo (FAO) Dkt.
Raphael Sallu wakati wa semina na waandishi wa habari uliofanyika leo jijini
Dar es salaam.
“Tatizo la kutumia vijiuasumu(Antibiotics) bila ya
kupata vipimo na ushauri kutoka kwa wataalamu wa afya limekua kubwa ambalo
linasababisha madhara ya kiuchumi na uhai kutokana na kuzidiwa na vimelea vya
ugonjwa ambavyo vinakua sugu kutokana na
matumizi mabaya ya dawa hapa nchini” alisema Dkt. Sallu.
Aidha, Dkt. Sallu amesema kuwa elimu ya kutumia
dawa bila ya kupata ushauri na vipimo kutoka kwa wataalamu wa afya ianze
kutolewa kuanzia ngazi za shule ya msingi na ngazi ya jamii kwa ujumla.
Mbali na hayo Dkt. Sallu amesisitiza kuwa
wanahabari wanatakiwa kuwa kipaumbele katika kuelimisha umma umuhimu wa kutumia
dawa kwa kufuata ushauri kutoka kwa wataalam kuhusu ugonjwa unaomsumbua pamoja
na matibabu yake.
Kwa upande wake Mratibu wa Taifa wa Mradi wa kupambana na na usugu wa vimelea
kutoka Shirika la Chakula (FAO) nchini Tanzania Dkt. Bachana Rubegwa amesema
kuwa katika kupambana na tatizo hili kunapaswa kuwepo na matumizi ya hali ya
juu ya chanjo ili kuweza kuepuka utumiaji hovyo wa dawa bila ya vipimo.
“Katika kupambana na utumiaji wa madawa bila ya
utaratibu mzuri ambao hauhusishi vipimo na ushauri kutoka kwa wataalamu wa afya
ni lazima maabara ya kutambua magonjwa sugu ijengwe nchini kwetu” alisema Dkt.
Bachana.
Hata hivyo Dkt. Bachana amesema kuwa wazilashaji
wa chakula na mifugo wanatakiwa kutumia dawa zinazostahili na sio kutumia antibiotics
katika mifugo yao pamoja na shughuli zao za kilimo ili kuepusha watanzania
walio wengi kutumia vyakula hivyo vyenye usugu wa vimelea vya magonjwa.
Mbali na hayo Dkt. Bachana ametoa rai kwa watoa
huduma za afya nchini kuacha kutoa dawa ambazo ni feki,zilizokwisha muda na
kuwashauri wananchi kuepuka matumizi ya dawa yasiyo ya lazima ili kuepuka usugu
wa vimelea vya ugonjwa kwenye miili ya watanzania.
Naye Mwakilishi kutoka Shirika la Afya Duniani
(WHO) upande wa kupambana na usugu wa vimelea vya magonjwa Dkt. Rose Shija
amesema kuwa watanzania wanatakiwa kutumia dawa sahihi na kwa wakati kadri
alivyoelekezwa na mtaalam wa afya ili kuepuka matatizo hayo na kujijengea afya
bora.
“Tubadili tabia katika kupunguza maambukizi
kupitia chanjo,kuosha mikono kwa maji safi yanayotiririka,kuepuka ngono zembe
na utunzaji salama wa chakula na sio kutumia dawa bila ya ushauri kutoka kwa wataalam
wa afya ili kuepuka usugu wa vimelea vya magonjwa mwilini” amesema Dkt. Shija.
0 on: "WATANZANIA WATAKIWA KUPATA VIPIMO VYA KITAALAM KABLA YA KUTUMIA DAWA."