Na WAMJWW
Mamlaka ya Chakula , Dawa na Vipodozi TFDA imetakiwa
kuboresha udhibiti wa uingizaji wa Dawa,
Vipodozi na Chakula nchini kiholela ili
kulinda afya ya Watanzania .
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii,
Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile wakati wa kuzindua CHETI CHA
MFUMO WA UHAKIKI UBORA WA HUDUMA KATIKA KIWANGO CHA KIMATAIFA CHA ISO 9001-2015
leo jijini Dar es Salaam.
“Dawa ni kitu nyeti sana, hatuwezi kuruhusu dawa
feki kuingia nchini, mnafanya kazi nzuri sana katika nyanja hii na muendelee na mpango huu ili kudhibiti
uingizaji wa vyakula visivyokidhi viwango na mahitaji ya watanzania, ” alisema
Dkt. Ndugulile.
Aidha Dkt. Ndugulile amesema kuwa TFDA wanatakiwa
kuzingatia muongozo wa kupitisha vyakula na vipodozi kwenye mipaka ya nchi kwa
kuzingatia ubora na viwango vilivyoweka katika kudhibiti uingizaji mbovu wa
vyakula.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa TFDA Bw. Hiiti
Silo amesema kuwa ili kuendelea kukidhi matakwa ya wateja na mahitaji yao
wameamua kuendana na kiwango cha kimataifa na kuwaita ISO kuja kuhakiki ambapo
wamefanikiwa kukidhi na kupata cheti.
“Shirika la Viwango la Kimataifa ISO limehakiki
ubora wa huduma zetu katika kukidhi mahitaji na matakwa ya watumiaji wa huduma
zetu na kutupatia cheti kinachoturuhusu kutoa huduma nchini” alisema Bw. Silo.
Aidha Bw. Silo amesema kuwa wapo bega kwa bega na
Serikali ya awamu ya tano ianyoongozwa na Rais Dkt. John pombe Magufuli katika
kusogeza mbele gurudumu la afya hapa nchini kupitia taasisi ya TFDA.
0 on: "TFDA IMETAKIWA KUBORESHA UDHIBITI WA UINGIZAJI WA VYAKULA NA DAWA KIHOLELA"