HOTUBA YA MHE. DR FAUSTINE NDUGULILE
(MB) NAIBU WAZIRI WA AFYA MAENDELEO YA JAMII JINSIA WAZEE NA WATOTO KATIKA
MKUTANO WA MWAKA WA MPANGO WA TAIFA WA KUDHIBITI KIFUA KIKUU NA UKOMA TAREHE 27
NOV -1 DISEMBA, 2017 MKOANI DODOMA
Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Muhammad
Bakari Kambi,
Mkurugenzi wa Kinga Dkt. Neema
Rusibamayila,
Naibu Meneja Mpango, Dkt. Liberate
Mleoh,
Wadau wa Maendeleo kutoka mashirika
mbali mbali ya kitaifa na kimataifa,
Waratibu wa Mpango wa Taifa wa Kudhibiti
Kifua Kikuu na Ukoma ngazi ya Taifa,
Waratibu wa Kifua kikuu na Ukoma wa Mikoa na wilaya
Wageni wetu waalikwa.
Mabibi na Mabwana
Awali
ya yote napenda niwapongeze kwa juhudi zenu za dhati kabisa katika kutekeleza
majukumu yenu ili kuhakikisha kuwa magonjwa ya kifua kikuu na ukoma yanadhibitiwa
na kuwa si tatizo la kiafya kwa watanzania.
Kama
mnavyofahamu tatizo la kifua kikuu katika nchi yetu ni kubwa. Kwa mujibu wa ripoti ya Shirika la Afya
Duniani (WHO) ya kifua kikuu ya mwaka 2017, Tanzania ni miongoni mwa nchi 30
duniani zenye kiwango kikubwa cha ugonjwa wa Kifua kikuu. Inakadiriwa kuwa
katika kila watanzania laki moja (100,000) watu mia mbili themanini na saba
(287) wanaugua kifua kikuu kwa mwaka. Utafiti wa kutathmini ukubwa wa tatizo la
Kifua kikuu nchini uliofanyika mwaka 2012/13 ulibaini kuwa kifua kikuu bado ni
tatizo kubwa katika maeneo ya vijijini na kwa wazee wenye umri zaidi ya miaka
60.
Vile vile, kutokana na ripoti ya kifua kikuu
ya Shirika la Afya Duniani ya mwaka 2017, Tanzania inakadiriwa kuwa na asilimia
1.3 ya wagonjwa wapya na asilimia 6.2 ya wagonjwa waliokwishatumia dawa za Kifua
kikuu wana Kifua kikuu sugu. Takwimu hizi zinaweka makadirio ya kuwepo wagonjwa
830 wa kifua kikuu sugu kwa mwaka 2016. Maambukizi mseto ya Kifua kikuu na
UKIMWI ni tatizo kubwa nchini ambapo asilimia 34 ya wagonjwa wa kifua kikuu
wana maambukizi ya VVU na asilimia 91 ya wagonjwa hao walianzishiwa dawa za
kufubaza VVU (ARV).
Kwa upande wa ugonjwa wa ukoma ni wazi kuwa
ukubwa wa tatizo la ukoma unaendelea kupungua. Kwa mujibu wa takwimu za Shirika
la Afya Duniani (WHO) za mwaka 2016 inaonyesha kuwa tuna chini ya mgonjwa mmoja
(0.4) katika kila watu 10,000.
Ndugu washiriki,
Miongoni
mwa mafanikio katika mapambano dhidi ya kifua kikuu nchini ni kuwa wagonjwa
wote wanaoanzishiwa matibabu, asilimia 90 wanapona kabisa, na asilimia 78 kati
ya hao wanapatiwa matibabu katika ngazi ya jamii. Vile vile asilimia 71 ya
wagonjwa wa Kifua kikuu sugu wanatibiwa na kupona kabisa.
Hata
hivyo changamoto kubwa tuliyonayo hapa nchini ni kuweza kuwaibua wagonjwa wote
wa Kifua kikuu cha kawaida na Kifua kikuu sugu ambapo kwa takwimu za sasa
zinaonyesha kuwa tunashindwa kuwafikia wagonjwa takriban 85,000 wa Kifua kikuu
na 600 wa Kifua kikuu sugu kwa mwaka. Vile vile mpaka sasa tumekwishagundua
wagonjwa wawili wa kifua kikuu sugu zaidi (XDR-TB) kwa miaka ya 2014 (ameshapona
kabisa) na 2017 yuko kwenye matibabu.
NdugU Washiriki
Wizara
kupitia Mpango inatekeleza Mpango Mkakati wa miaka mitano wa Kudhibiti Kifua
kikuu na Ukoma (2015-2020). Mikakati iliyowekwa ili kukabiliana nazo ni pamoja
na:-
·
Kuhakikisha dawa za kutibu Kifua kikuu zinaendelea kupatikana
wakati wote na bila malipo yoyote
·
Kuimarisha uwezo wa vituo vya ugunduzi wa Kifua
kikuu kwa kutumia teknolojia mpya ya
vipimo kwa kutumia vinasaba vya GeneXpert MTB/RIF,
·
Kuimarisha uwezo wa maabara za kikanda
zilizopo Dodoma, (Dodoma Hospitali) Mwanza, (Bugando) Mbeya (Mbeya Rufaa) na
Kilimanjaro (Kibong’oto),
·
Kushirikisha sekta binafsi katika mapambano dhidi ya Kifua kikuu
ikiwemo maduka ya dawa muhimu, famasi na hospitali binafsi katika kuibua
wagonjwa wa Kifua kikuu,
·
Kuimarisha mikakati ya uibuaji wagonjwa wa Kifua kikuu kutoka
kwa wachimbaji wadogo wadogo wa madini na jamii zinazowazunguka kwa
kushirikiana na wadau mbali mbali,
·
Uboreshaji wa huduma za uibuaji wa wagonjwa kupitia
ushirikishwaji wa vitengo vyote katika vituo vya kutolea huduma za afya,
·
Kushirikisha jamii katika kuibua wahisiwa wa Kifua kikuu na Ukoma
na kuwapeleka kwenye vituo vya kutolea huduma za afya kwa uchunguzi na tiba
·
Kuimarisha mikakati ya uibuaji watoto wenye maambukizi ya Kifua
kikuu na kuanzisha dawa mpya za Kifua kikuu kwa watoto,
·
Kugatua huduma za Kifua kikuu sugu kwa kushirikisha vituo
vingine zaidi ya Hospitali ya Magonjwa ya Kuambukiza ya Kibong’oto na kuanzisha matibabu ya muda mfupi ya Kifua kikuu sugu
kutoka miezi 24 hadi miezi 9,
·
Kuimarisha mfumo wa ukusanyaji wa taarifa za Mpango kwa mfumo wa
kielektroniki.
Kwa
upande wa ugonjwa wa Ukoma, ni wazi kuwa, ukubwa wa tatizo la ugonjwa huo
linapungua kila mwaka na waathirika wengi bado tunawapata wakiwa tayari
wamepata ulemavu. Kuna watanzania wenzetu takribani 300 kila mwaka hupata
ulemavu wa kudumu utokanao na ukoma; ulemavu huu unazuilika kabisa. Takwimu za
Mpango za mwaka 2015 zinaainisha kuwa wilaya ambazo bado zina wagonjwa wengi wa
ukoma ni Masasi, Nanyumbu, Namtumbo, Liwale, Ruangwa, Mkinga, Kilombero, Chato
na Nkasi. Hivyo basi ni jukumu letu sote
kuongeza juhudi za kupambana na Ukoma kwa kuongeza ubunifu katika kutafuta njia
na mbinu mpya za kuhakikisha wagonjwa wanagunduliwa mapema na kupatiwa matibabu
kwa wakati.
Miongoni
mwa mafanikio yaliyopatikana katika kudhibiti Ukoma nchini ni pamoja na:
·
Asilimia 95 ya wenye Ukoma hafifu na asilimia
93 ya wenye ukoma mkali walioanzishiwa matibabu walipona kabisa
Ndugu Waratibu,
Nitoe rai kwa mikoa na
wilaya kushirikisha wadau wote katika kutekeleza mikakati iliyoainishwa na
Mpango ambayo inalenga kutimiza malengo ya kitaifa ya kudhibiti Kifua kikuu
kitaifa na kidunia.
Ni
matumaini yangu kwamba mkutano huu utakuwa ni chachu ya kuibua changamoto
tulizo nazo, kujifunza kutoka kwa kila mmoja wetu na hivyo basi kuweza
kuimarisha mipango na mikakati yetu ili tuwapatie wananchi huduma bora na
endelevu. Ni jukumu la kila mmoja wetu kuhakikisha wagonjwa wenye Kifua kikuu
na ukoma wanaibuliwa na kupatiwa matibabu kwa wakati. Kila mtumishi atimize
wajibu wake.
Napenda
kusisitiza na kuwaasa juu ya utekelezaji bora wa kazi za Mpango na matumizi sahihi
ya fedha zinazofadhiliwa na wadau wetu wa maendeleo na kuzitolea taarifa kwa
wakati ili kuendana na kasi ya Serikali ya awamu ya tano, yaani “HAPA KAZI TU”
Ndugu Waratibu,
Serikali
inapenda kuchukua fursa hii kuwashukuru wadau wa maendeleo kama vile Global
Fund ATM, Shirika la Afya Duniani (WHO) Serikali ya Marekani kupitia USAID na mashirika
yanayotekeleza shughuli za Kifua kikuu nchini kwa juhudi zao za kuisaidia
serikali katika kupambana na magonjwa haya. Mchango wenu ni muhimu sana katika
kuhakikisha mikakati tuliyojiwekea inatekelezwa kwa ufanisi na kwa wakati.
Ndugu washiriki, Mabibi na Mabwana
Nichukue
fursa hii kutamka kuwa mkutano huu wa Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Kifua kikuu
na Ukoma kwa mwaka 2017 umefunguliwa rasmi.
Mungu ibariki Africa Mungu ibariki
Tanzania Asanteni kwa kunisikiliza.
0 on: "HOTUBA YA MHE. DR FAUSTINE NDUGULILE (MB)"