JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO
TANZANIA KUWA MNUNUZI MKUU WA DAWA NA VIFAA TIBA UKANDA WA SADC
Mawaziri
wa Afya wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa
Africa (SADC) kwa kauli moja wamepitisha uteuzi wa nchi ya Tanzania
kupitia Bohari ya Dawa (MSD) kuwa Mnunuzi Mkuu wa Dawa, Vifaa Tiba na
Vitendanishi vya Maabara kwa ajili ya nchi hizo kupitia mfumo wa Ununuzi
Shirikishi (SADC Pooled Procurement Services (SPPS).
Uteuzi
huo wa nchi ya Tanzania umepita bila kipingamizi mwishoni mwa wiki
kwenye Mkutano wa Mkutano wa Mawaziri wa Afya wa nchi za SADC
uliowakutanisha Mawaziri wa Afya na Mawaziri wanaohusika na masuala ya
UKIMWI uliofanyika mjini Polokwane, Limpopo – Afrika Kusini.
Hatua
ya uteuzi wa Tanzania kuwa mnunuzi mkuu wa Dawa, Vifaa Tiba na
Vitendanishi vya Maabara umetokana na juhudi za Mhe. Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Mhe. John Pombe Magufuli kuimarisha hali ya
upatikanaji wa dawa MSD ambapo sasa inatekeleza majukumu yake kwa
ufanisi mkubwa .
Aidha,umahiri
na uzoefu wa Bohari ya Dawa (MSD) katika masuala ya ununuzi, utunzaji
na usambazaji Dawa, Vifaa Tiba na Vitendanishi vya Maabara (yaani
mnyororo wa ugavi) unaeleweka na kuaminika vizuri hata na nchi nyingine
zilizowahi kututembelea kujifunza na kubadilishana uzoefu.
Kwa hatua hiyo MSD itakuwa na dhamana na majukumu yafuatayo:
Kununua Dawa na Vifaa Tiba kwa ajili ya nchi za SADC
Usimamizi wa taarifa na takwimu za Dawa na Vifaa Tiba vitakavyohitajika
Usimamizi
wa kanzidata (Database) ya dawa za nchi wananchama wa SADC na usimamizi
wa bei elekezi ya Dawa, Vifaa Tiba na Vitendanishi vya Maabara
Kusimamia manunuzi ya Dawa, Vifaa Tiba na Vitendanishi vya Maabara kwa ajili ya Ukanda wa SADC na kusimamia mnyororo wa ugavi
Kutoa huduma za kitaalamu na kupanga bei elekezi na
Kutoa huduma za ushauri wa kitaalam katika masuala ya dawa na vifaa tiba.
Hatua
hii itapunguza kwa kiasi kikubwa bei ya dawa na vifaa tiba kwa ajili ya
matumizi ya nchi wananchama wa SADC. Jambo ambalo limeipatia heshima na
sifa kubwa Tanzania, kwani imeaminiwa kufanya ununuzi wa dawa kwa niaba
ya nchi nyingine kumi na tano (15) ambazo ni wanachama wa SADC.
Tanzania
kupewa jukumu hilo ni jambo la kujivunia sana tena inaonyesha dhahiri
tumetambulika tuko vizuri kwenye masuala mazima ya mnyororo wa ugavi kwa
nchi wanachama wa SADC.
Faida zitakazopatikana kwa Tanzania kuwa Mwenyeji wa huduma hii ni kama zifuatazo:
Heshima kwa nchi yetu kwa kuaminiwa na nchi wanachama wa SADC baada ya kukidhi vigezo vya kitaalam
Viwanda
vyetu vya ndani vitaweza kuuza dawa zao kwa nchi za SADC, kwani wajumbe
wa mkutano tumekubaliana kuwa na kituo kimoja kitakachoshughulikia
udhibiti ubora na ukaguzi
Bei ya dawa itapungua zaidi maana sasa tutaweza kwenda moja kwa moja
kwa wazalishaji sio kama nchi (Tanzania), lakini kama Ukanda
unaoshughulikia nchi 15
Itaongeza ajira na kuijengea uwezo Bohari ya dawa(MSD)
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano Serikalini-Afya
16/11/2017
0 on: " TANZANIA KUWA MNUNUZI MKUU WA DAWA NA VIFAA TIBA UKANDA WA SADC"