Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt.
Faustine Ndugulile (kushoto) akitoa kingatiba kwa mtoto aliyekuwa
akiishi na mgonjwa wa ukoma. Kingtiba hiyo itamlinda dhidi ya ugonjwa wa
ukoma imezinduliwa na Dkt. Ndugulile katika maadhimisho ya siku ya
Ukoma Duniani yaliyofanyika Wilayani Mvomero, Morogoro.
Baadhi ya Wanafunzi waliofika kusikiliza ujumbe kuhusu Ugonjwa wa Ukoma na kupata Kingatiba ya kuzuia ugonjwa huo ilikuwa ikitolewa katika viwanja vya kijiji cha Chazi, vilivyopo Wilaya ya Mvomero Mkoa wa Morogoro.
Wazee waliopata msaaada wa
viatu vya kutembelea toka Taasisi ya GLRA inayowasaidai watu wenye
ugonjwa wa ukoma nchini, wakifuatilia kwa makini, ujumbe kutoka kwa mgeni rasmi Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt.
Faustine Ndugulile katika siku ya Ukoma Duniani.
Wakina mama wa Kijiji cha Chazi, Mvomero , Mkoa wa Morogoro wakifuatilia kwa makini, ujumbe kutoka kwa
mgeni rasmi Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na
Watoto Dkt.
Faustine Ndugulile katika siku ya Ukoma Duniani.
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt.
Faustine Ndugulile (Wapili kushoto) akifuatilia kwa makini risala kutoka kwa Mwakilishi wa Wazee wenye ulemavu wanaoishi na Ukoma katika kijiji cha Chazi, Wilaya ya
Mvomero Mkoani Morogoro
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt.
Faustine Ndugulile (kulia)akisalimiana na Mzee Anthony Martin (kushoto)
wakati alipotembelea makazi ya wasiojiweza ya Chazi, Katika Wilaya ya
Mvomero Mkoani Morogoro
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na
Watoto Dkt.
Faustine Ndugulile akishika kito cha Mtumbwi katika moja kati ya banda la maonesho katika kijiji cha Chazi, Wilaya ya
Mvomero Mkoani Morogoro
Picha ya pamoja, Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,
Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulike (wa nne kutoka kushoto,
walioketi) akiwa na wadau wa Sekta ya Afya nchini.
UKOMA HAUNA UHUSIANO NA IMANI ZA KISHIRIKINA - SERIKALI
Na WAMJW -Mvomero, Morogoro.
“Ugonjwa
wa ukoma hausababishwi na imani za kishirika bali ni vimelea vya
magonjwa ambavyo huingia ndani ya mwili na kusababisha ukoma”
Hiyo
ni kauli ya Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na
Watoto Dkt. Faustine Ndugulile alipokuwa akizungumza na waathirika wa
ugonjwa wa ukoma pamoja na wananchi katika maadhimisho ya siku ya Ukoma
Duniani, wilayani Mvomero, katika Mkoa waMorogoro.
Dkt.
Ndugulile amewaasa wananchi kuachana na imani za kishirikina kwa
kuamini kuwa ya kwamba ugonjwa huo unahusika moja kwa moja na imani hizo
za giza.
“Dhana ya
kwamba ugonjwa huu ni wa kurogwa siyo kweli, ugonjwa wa ukoma
hausababishwi na mtu kulogwa wala kutupiwa jini bali ni vimelea ambavyo
huingia mwilini na kusababisha ugonjwa wa ukoma, ni watu kama mimi na
wewe” anasema Dkt Ndugulile.
Aidha
Dkt Ndugulile ametumia nafasi hiyo kuwaelimisha wananchi kuwa ugonjwa
wa ukoma unatibika na kusema kuwa dawa za kutibu ugonjwa huo zipo na
kuwaondolea hofu ya kuwa ugonjwa huo kutotibika. Hata hivyo Dkt.
Ndugulile ametoa rai kwa wananchi wote kujitokeza mapema katika vituo
vya kutolea huduma za afya kupata huduma za matibabu pindi wanapohisi
kuwa na dalili za ugonjwa wa ukoma.
“Mtu
yeyote ambaye anaanza kuona mabadiliko kwenye ngozi yake, anapata
mabaka ambayo hayaelewi au kupoteza hisia pindi unapojigusa ni muda wa
kwenda hospitalini kufanya uchunguzi na kama utagundulika kuwa na
vimelea vya ugonjwa wa ukoma utapewa matibabu” alisisitiza Dkt.
Ndugulile.
Dkt. Ndugulile
amewataka wananchi kuwa mabalozi wa kuwaelimisha watu wengine juu ya
dalili na athari za ugonjwa wa ukoma. “Niwaombe ndugu wananchi tuendelee
kutoa elimu kuhusiana na ugonjwa huu ni ugonjwa ambao tunaweza
tukauzuia na tusiwe na athari kwenye jamii na tusingependa kuona kwenye
zama hizi watu wanapata athari za kudumu na wanapoteza viungo, hisia
katika sehemu za miili yao au kuharibika ngozi kwa sababu ya kutopata
matibabu mapema” alifafanua Dkt Ndugulile.
Naibu
Waziri huyo wa Afya amesema kuwa Serikali ipo katika hatua nzuri za
kutokomeza ugonjwa wa ukoma nchini licha ya changamoto ambazo zipo
katika baadhi ya maeneo sugu ambayo ugonjwa huo umeonekana kuwa ni
tatizo. “Takwimu zinaonyesha kuwa takribani watu 1993 huugua ugonjwa wa
ukoma kila mwaka huku mikoa ya Lindi, Rukwa, Mtwara, Pwani, Tanga,
Geita, Dodoma, Tabora, Kigoma na Mkoa wa Morogoro ikiwa na idadi kubwa
ya wagonjwa” alisema Dkt. Ndugulile.
Sasa
hivi tumepiga hatua kubwa, tunajua jinsi gani ugonjwa unaambukizwa, na
namna ya kuutibu pamoja na kujikinga dhidi ya maambukizi mapya, naamini
kwa mikakati iliyopo tunaweza kuutokomeza ugonjwa huu.
Akizungumiza
mikakati iliyopo Dkt Ndugulile amesema kuwa pamoja na elimu ambayo
wamekuwa wakiitoa, Serikali imehamishia nguvu kwenda kwenye jamii moja
kwa moja kuwabaini wagonjwa wa ukoma. “Hatusubiri watu watufate,
tumewekeza nguvu nyingi kwenye jamii na kuwafikia huko huko maeneo
wanayoishi” alisema Dkt Ndugulile.
Kwa
upande mwingine, Dkt Ndugulile amezindua Mpango wa Kingatiba ya Ugonjwa
wa Ukoma mahususi kwa wale ambao wamekuwa wakiishi na wagonjwa wa ukoma
ili waweze kujikinga kutopata ugonjwa huo na kutoa rai kwa wananchi
wote ambao wamekuwa wakiishi na wagonjwa wa ukoma kujitokeza katika
vituo vya huduma za afya kumeza dawa hizo za kujikinga na ukoma.
“Mtu
mwenye ukoma na ambaye amekunywa dawa za kingatiba hawezi kusambaza
ugonjwa huu na tunaweza kuishi na kushirikiana naye kufanya shughuli
mbalimbali kimaendeleo” alisema Dkt Ndugulile na kuwaasa wananchi kuacha
tabia za kuwanyanyapaa wenye ukoma.
Dkt
Ndugulile ameipongeza taasisi ya GLRA kutoka Ujerumani inayojihusisha
na kuwatunza watu wenye ukoma kwa kuwaanzishia miradi ya ujasiriamali na
kuwaunganisha wahanga wa ugonjwa huo na jamii pamoja na kuwapongeza pia
wagonjwa wa ukoma kujishughulisha na shughuli za uzalishaji kipato
kuliko kuwa omba omba barabarani.
Awali
akitoa salamu zake Rais wa Taasisi ya GLRA Bw. Patric Meisen amesema
kuwa anafuraha kuona Tanzania na Ujerumani zikiwa na mahusiano mazuri na
kuahidi kuendelea kuwasaida waathirika wa ugonjwa ukoma nchini.
“Tumekuwa
tukifanya kazi na wataalam wa afya katika kuwatunza waathirika
waugonjwa wa ukoma, hatujaishia hapo tuu, tumewasaidia waathirika wa
ugonjwa huu kwa kuwapatia mitaji itakayowasaidia kujiongezea kipato
ambacho kitawasaidia” alisema Bw. Meisen.
Siku
ya Ukoma Duniani huadhimishiwa kila jumapili ya mwisho wa mwezi
Januari, ambapo kwa mwaka huu 2019, maadhimisho hayo kitaifa yamefanyika
Wilayani Mvomero, Mkoa wa Morogoro yakiwahusisha wadau mbalimbali wa
Sekta ya afya huku kauli mbiu ikiwa ni *“Tutokomeze Ubaguzi, Unyanyapaa
na Chuki dhidi ya Waathirika wa Ukoma”*
Mwisho