Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy
Mwalimu akitoa maelekezo kwa Injini mkuu wa TBA Simiyu Bw. Likimaitare
Naunga wakati akipotembelea ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa
Simiyu. Kulia ni Mkuu wa mkoa huo Bw. Anthony Mtaka.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy
Mwalimu akimsalimia ndugu wa mgonjwa aliyelazwa (jina halijafahamika)
katika hospitali teule ya Somanda alipotembelea hospitali kuona hali ya
utaoaji huduma za afya. Kulia ni Mwenyekiti wa CCM wilaya Bi. Juliana
Mahongo na Daktari zamu.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy
Mwalimu akisisitiza jambo wakati alipotembelea wodi za Hospitali ya
rufaa ya mkoa wa Simiyu. Kushoto ni Mganga Mkuu wa mkoa Dkt. Mageda
Kihulya, Mbunge wa bunge la Afrika Mashariki Bi. Happines Lugiko na Mkuu
wa Mkoa wa Simiyu Bw. Anthony Mtaka.
TBA WAPEWA WIKI MBILI KUPELEKA FEDHA ZA UJENZI WA HOSPITALI YA RUFAA YA MKOA WA SIMIYU
Na WAMJW-SIMIYU
Waziri
wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu
ameiagiza wakala wa ujenzi (TBA) kupeleka fedha za ujenzi zilizotolewa
na Serikali katika ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Simiyu
kuhakikisha zinafika ndani ya wiki mbili.
Agizo
hilo limetolewa leo wakati alipotembelea ujenzi wa jengo la Uchunguzi
na jengo la Mama na Mtoto na kutoridhishwa na kasi ya ujenzi huo huku
sababu kubwa inayopelekea kusuasua ikitajwa ni fedha kidogo
zilizopokelewa na wakala wa ujenzi wa mkoa wa Simiyu kiasi cha Shilingi
Milioni 430 wakati serikali imetoa Bilioni 1.064 kwa ajili ya ujenzi
huo.
“Ninawashngaa TBA
kwanini wanakaa na fedha wakati wanajua mradi wa ujenzi unaendelea huku,
serikali imetoa Bilioni 1.064 ili zitumike katika ujenzi wa Hospitali
hii lakini TBA wameleta milioni 430 tu, hizo fedha zingine ziko wapi?”.
Alihoji waziri Ummy.
Kufuatia
hali hiyo Waziri Ummy ameahidi kushughulikia suala hilo na kuahidi
fedha hizo zitafika katika mradi huo ndani ya wiki mbili ili ziweze
kusaidia kuongeza kasi ya ujenzi wa majengo hayo ambapo yanatarajiwa
kukabidhiwa na kuanza kutoa huduma kuanzia mwezi Juni mwaka huu.
Kwa
upande wake Injinia mkuu wa TBA anayesimamia ujenzi huo Bw. Likimaitare
Naunga amesema fedha zilizoletwa katika mradi huo hazitoshi na ndiyo
sababu kubwa inayochangia kusuasua kwa mradi huo huku akitaka wakala wa
ujenzi (TBA) kuhakikisha fedha hizo zinafika mapema ili zisaidie
kuongeza kasi ya mradi na kufikia lengo.
Naye
Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Bw. Anthony Mtaka amemuahidi Waziri Ummy kuwa
atasimamia kwa karibu upatikanaji wa fedha hizo zilizopo TBA zinafika
katika mradi na kuhakikisha mradi unakamilika ndani ya muda uliopangwa
ili huduma muhimu za kibingwa zianze kutolewa Hopitalini hapo.
Wakati
huo huo waziri Ummy ametembelea Hospitali teule ya Somanda iliyopo
wilayani Bariadi na kuonekana kutoridhishwa na huduma zinazotolewa
katika jengo la Mama na Mtoto ambapo alishuhudia huduma mbaya
zinazotolewa kwa akinamama wajawazito na watoto wachanga.
Pia
Waziri Ummy ameshangazwa baada ya kuona hakuna chumba cha kuhifadhia
watoto wenye uhitaji wa huduma maalum kama huduma za joto kwa watoto
waliozaliwa kabla ya muda (Njiti) na kuitaka Hospitali hiyo kuwa na
chumba hicho muhimu.
Aidha,
Waziri Ummy ameshangazwa na kutokuwepo kwa huduma za upasuaji katika
jengo hilo huku sababu ikitajwa kutokuwepo kwa Sinki, hali
inayosababisha usumbufu mkubwa kwa akinamama wajawazito wanaofika kupata
huduma hospitalini hapo.
Kufuatia
hali hiyo waziri huyo ametoa siku tatu kwa uongozi wa Hospitali hiyo
chini ya Mganga Mkuu wa Mkoa Dkt. Mageda Kihulya kuhakikisha wananunua
sinki hilo na huduma za upasuaji zianze kutolewa mara moja katika jengo
hilo.
Waziri Ummy yupo
Mkoani hapa katika ziara ya kikazi ya kutembelea mikoa ya Simiyu,
Geita na Shinyanga ili kuweza kuona hali ya miundombinu na utoaji huduma
katika hospitali za rufaa za mikoa.
0 on: "TBA WAPEWA WIKI MBILI KUPELEKA FEDHA ZA UJENZI WA HOSPITALI YA RUFAA YA MKOA WA SIMIYU"