Like us on Facebook

Inaendeshwa na Blogger.

Tafuta katika Blogu Hii

Kumbukumbu la Blogu

Instagram

visitors

display number of visitors

Popular Posts

Pages

Flickr Images

Jumapili, 27 Januari 2019

UKOMA SI UGONJWA WAKURITHI AU KUROGWA



Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu akisalimiana na Wazee ambao Waathirika wa ugonjwa wa Ukoma katika Kambi ya Wazee Nunge, Kigamboni Jijini Dar es salaam.

Na WAMJW - DSM

Jana nilitembelea Makazi ya Wazee Nunge, Kigamboni jijini Dar es salaam, ambapo pia nimepeana mikono na waathirika wa Ukoma ikiwa ni ishara ya kutekeleza kwa vitendo kauli mbiu yetu ya maadhimisho ya Siku ya Ukoma 2019 ni Tutokomeze Ubaguzi, Unyanyapaa na Chuki dhidi ya Waathirika wa Ukoma.
Katika maadhimisho haya ninapenda kuwakumbusha watanzania kuwa, ukoma bado ni tatizo katika nchi yetu. Kwa mujibu wa Takwimu za 2017, jumla ya wagonjwa wapya 1,933 waligundulika kuwa na ukoma na hivyo kufanya kiwango cha ukoma kuwa watu 4 kwa kila watu 100,000. Takwimu hizi zinaifanya Tanzania kuendelea kuwa  miongoni mwa nchi 22 zenye wagonjwa wengi wa ukoma duniani. Nchi nyingine ni India, Indonesia, Brazil, Ethiopia, Msumbiji, Nigeria na DRC Congo.

Aidha kuna mikoa 10 ambayo hugundua wagonjwa wapya wengi zaidi. Mikoa hii ni Lindi, Mtwara, Pwani, Morogoro, Tanga, Dodoma, Geita, Kigoma, Rukwa na Tabora. Aidha zipo Wilaya 20 zenye kiwango kikubwa cha wagonjwa wapya wa Ukoma ambazo ni; Liwale, Lindi Vijijini, Nachingwea, Ruangwa, Nanyumbu, Masasi Mjini, Pangani, Mkinga, Korogwe, Mvomero, Kilombero, Morogoro Vijijini, Ulanga, Shinyanga Manispaa, Chato, Mafia, Rufiji, Kilwa, Nkasi na Mpanda.

Serikali kwa kushirikiana na wadau tutaendelea kuchukua hatua mbalimbali kuhakikisha ukoma unatokomezwa nchini. Hivyo nitoe wito wangu kwa jamii, wazazi na walezi kujenga tabia ya kuchunguza miili yetu na ya watoto wetu. Endapo utaona mojawapo ya dalili za ukoma ni muhimu kwenda kituo cha Tiba kwa uchunguzi bila kuchelewa. Dalili za Ukoma ni baka au mabaka mwilini yenye rangi ya shaba na hayana hisia, vijinundu kwenye ngozi au mishipa ya fahamu kuvimba, ganzi kwenye mikono au miguu.

Ugonjwa wa ukoma unatibika. Mgonjwa aliyeanza tiba hawezi kuambukiza mtu mwingine hivyo hakuna sababu ya kumtenga. Tiba ya Ukoma inapatikana nchini kote na hutolewa bila malipo kwa wagonjwa wote.
Aidha, ninaitaka jamii kuachana na imani potofu kuwa ukoma ni ugonjwa wa kurithi au kulongwa. Ukoma ni ugonjwa wa kuambukiza unaosababishwa na vimelea vinavyoshambulia mishipa ya fahamu na huambukizwa kwa njia ya hewa pekee! Aidha ninawataka wagonjwa wa ukoma kuacha kuchelewa kujitokeza kupata matibabu hadi wanapopata ulemavu.

“Nirudie tena kusisitiza pale tunapoona mabadiliko yoyote yanajitokeza kwenye miili yetu twende mapema ktk vituo vya Tiba kuchunguzwa ili tupate matibabu” Nimalizie kwa kuwashukuru watoa huduma katika vituo vya afya kote nchini kwa juhudi kubwa wanazofanya kila siku kuhakikisha ugonjwa wa ukoma unatokomezwa nchini. 
Ninawashukuru wanahabari kwa kuendelea kuelimisha jamii kuhusu magonjwa mbalimbali ikiwemo ukoma. Pia, ninayashukuru mashirika mbalimbali ya ndani na nje ya nchi yanayounga mkono juhudi zetu za kutokomeza ukoma nchini.

“Tutokomeze Ubaguzi, Unyanyapaa na Chuki dhidi ya Waathirika wa Ukoma”.

Ummy Mwalimu, Mb
WAMJW
27 Jan. 2019.

0 on: "UKOMA SI UGONJWA WAKURITHI AU KUROGWA"