Mkuu wa Wilaya ya Songea mhe. Pololeti Mgema akimkaribisha mgeni rasmi Naibu Waziri wa Afya Dkt. Ndugulile (hayupo kwenye picha) ili aweze kuzungumza na wanafunzi na uongozi wa chuo cha Afisa tabibu COTC Songea,
Na WAMJW - RUVUMA
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile amewaagiza watendaji wa Halmshauri zote nchini kutotumia wakandarasi katika kujenga miradi inayohusu Sekta ya Afya na Maendeleo ya Jamii nchini, bali kutumia mtindo wa 'Forced Account' (kuwahusisha mafundi wa kawaida katika kujenga miradi hiyo)
Agizo hilo limetolewa mkoani Ruvuma wakati alipotembelea na kujionea ukarabati na ujenzi katika Chuo cha Wauguzi Songea na Chuo cha Maendeleo ya Jamii wakati alipofanya ziara ya kukagua hali ya utoaji huduma za Afya na Maendeleo ya Jamii mkoani hapo.
Dkt. Ndugulile amefikia hatua hiyo baada ya kupokea taarifa ya kuanza kwa mchakato wa ujenzi wa baadhi ya majengo na ukuta wa Chuo cha Afisa tabibu (COTC - Songea) mkoani humo ambao unagharimu zaidi ya Shilingi millioni 900 ambazo fedha hizo zingetumia mtindo wa 'Forced Account' zingejenga majengo mengi zaidi na ukuta.
Aidha, Dkt. Ndugulile ameongeza kuwa katika zama hizi, Serikali ya Awamu ya Tano itazingatia na kufuatilia matumizi sahihi ya fedha za miradi ya Maendeleo na Wizara itasimamia kwa karibu Miradi hiyo.
"Niseme tu ni marufuku kutumia wakandarasi katika kutekeleza miradi inayohusu Wizara hii niliyopo labda muyafanye haya wakati mimi sipo" alisisitiza Dkt. Ndugulile.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Songea Mhe.Pololeti Mgema amemuahidi Naibu Waziri huyo kusimamia uendeshaji wa vyuo vyote vilivyopo katika Wilaya yake kwa ukaribu.
Akitoa taarifa ya ujenzi na ukarabati wa Chuo cha Wauguzi Songea Kaimu Mkuu wa Chuo hicho Dkt. Geoffrey Mdede amesema Chuo kinakabiliwa na changamoto za miundombinu pamoja na upungufu wa wakufunzi ambapo mpaka sasa kuna wakufunzi saba wanaofundisha jumla ya wanafunzi 105.
MWISHO.
0 on: "SERIKALI YAPIGA MARUFUKU MATUMIZI YA WAKANDARASI UTEKELEZAJI MIRADI KATIKA SEKTA YA AFYA NA MAENDELEO YA JAMII NCHINI."