Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt Faustine Ndugulile(mwenye shati jeupe) akikata utepe wakati wa uzinduzi wa Zahanati ya St. Mary's Mivumoni wilayani Pangani, Tanga. Kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Pangani Bi. Zainab Abdallah Issa, aliye kulia ni Mhashamu Baba Askofu Anthony Banzi wa Kanisa Katoliki Jimbo la Tanga.
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt Faustine Ndugulile (kushoto) akipokea pongezi toka kwa Mhashamu Baba Askofu Athony Banzi wa Jimbo Katoliki Tanga (kulia) mara baada ya kuzindua Zahanati ya St. Mary's Mivumoni iliyopo katika Wilaya ya Pangani Mkoani Tanga
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt Faustine Ndugulile akipokea baraka toka kwa Mhashamu Baba Askofu Banzi wakati wa misa ya kubariki Zahanati ya St. Mary's Mivumoni iliyoko Wilayani Pangani, Tanga.
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt Faustine Ndugulile akikagua vifaa katika Zahanati ya St. Mary's Mivumoni iliyoko WIlayani Pangani, Tanga mara baada ya kuizindua.
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt Faustine Ndugulile (kushoto) akisalimiana na Mkuu wa WIlaya ya Pangani Bi. Zainab Abdallah Issa (kulia) mara baada ya kuwasili wilayani humo tayari kwa ziara ya kikazi.
NA WAMJW - Pangani, TANGA.
Pamoja na juhudi zinazofanywa na Serikali kuboresha sekta ya afya nchini, Taasisi za Dini bado ni wadau wakubwa wanaotegemewa na Serikali kuboresha Sekta hiyo kutokana na uwekezaji mkubwa wa miundombinu pamoja na utoaji wa huduma ya afya nchini.
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile alipokuwa akizindua Zahanati ya St. Mary Mivumoni, inayomilikiwa na Masista wa Mtakatifu Francis wa Capuchin katika Kata ya Bushiri, Wilayani Pangani, Mkoa wa Tanga.
Dkt Ndugulile amesema kuwa Taasisi za Dini zina mchango mkubwa kwa maendeleo ya wananchi, kutokana na huduma za kijamii kama vile elimu na afya ambazo zimekuwa zikitolewa na madhebeu ya dini mbalimbali nchini na kusema kuwa Serikali itaendelea kutoa ushirikiano wa kutosha kuhakikisha ushirikiano uliopo unaleta manufaa kwa wananchi.
Akitaja takwimu za idadi ya vituo vya kutolea huduma za afya nchini, Dkt Ndugulile amesema kuwa “Takwimu zinaonyesha kuwa katika Sekta ya Afya, makanisa yana zahanati zaidi ya 791, vituo vya afya 160 pamoja na hospitali 116” na kuendelea “huu ni mchango mkubwa sana ambao haupaswi kupuuzwa bali kuenziwa na sisi tunashukuru sana” alisikika akisema Dkt. Ndugulile.
Aidha baada ya ukaguzi wa jengo hilo la zahanati, Dkt Ndugulile amefurahishwa kuona zahanati hiyo ina vifaa vya kisasa ambavyo vinaifanya kituo hicho kuvuka sifa za kuwa zahanati kutaka mchakato wa kuipandisha kuwa kituo cha afya huku uongozi wa zahanati hiyo ukiombwa kushughulikia suala la kuboresha miundombinu ya majengo ili kupata wodi za kulaza wagonjwa.
“Zahanati mliyojenga ni kubwa, nzuri na ina nafasi, tutakuwa hatujatenda haki kama tutaiacha ikiwa katika ngazi ya zahanati, tuweke malengo ya kuifanya kuwa kituo cha afya unaanza ili huduma nyingi za matibabu ziwe zinapatikana katika eneo hili” Alisema Dkt Ndugulile.
Kwa upande wake Mhashamu Baba Askofu Anthony Banzi wa Jimbo Katoliki Tanga amesema kuwa ni jambo la faraja kuona Taasisi za Dini zikishirikiana na Serikali katika kutoa huduma kwa jamii.
“Tunaishukuru sana Serikali kwa kutoa nafasi kwa mashirika ya dini kuweza kushirikiana na Serikali katika kutoa huduma kwa jamii zikiwemo elimu, afya pamoja na huduma nyingine” alisema Mhashamu Baba Askofu Anthony Banzi.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Pangani Bi zainab Abdallah Issa amesema kuwa uwepo wa zahanati hiyo itawasaidia wakazi wa mivumoni na Tarafa ya Madanga kwa ujumla kupata huduma za afya karibu na maeneo yao tofauti na awali ambapo walikuwa wanatumia muda mwingi kusafiri umbali mrefu kufata huduma za afya.
Kwa upande mwingine Dkt Ndugulile ametumia jukwaa hilo kuzungumzia mikakati iliyopo katika kuboresha sekta ya afya kwa upande wa bima ya afya ambapo amesema kuwa Serikali iko mbioni kuboresha mifumo ya bima ya afya itakayoiwezesha mwananchi mmoja na mwenza pamoja na wategemzi wanne kupata huduma za afya kwa gharama za shilingi 30,000, fedha ambayo itawaweza kupata huduma za matibabu kuanzia ngazi ya zahanati hadi hospitali ya Mkoa na kutoa rai kwa wananchi kujitokeza kwa wingi kukata bima ya afya pindi utaratibu huo utakapo anza rasmi.
0 on: "TAASISI ZA DINI NI WADAU WAKUBWA WA SEKTA YA AFYA NCHINI"