Meneja Uhusiano wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) Bi. Angela
Mziray akizungumza wakati wa ziara maalum ya Maafisa habari wa Wizara ya
Afya na taasisi zake katika kampeni maalum ya ‘Tunaboresha Sekta ya
Afya’ inayolenga kueleza mafanikio makubwa yaliyofikiwa katika kipindi
cha miaka mitatu ya Serikali ya awamu ya tano chini ya Rais Dkt. John
Magufuli. leo 11.1.2019, Makao makuu ya Mfuko huo Jijini Dar es Salaam
Afisa wa kitengo cha Tehama Charles Madangi Charles akionesha namna ya mfuko wa kisasa unavyofanya kazi katika kitengo cha tehama
Msimamizi wa nyaraka wa NHIF, Erasto Msigwa akieleza namna mfumo huo unavyofanya kazi wa kutunza kumbukumbu kwa njia ya kisasa
Sabrina Mponda wa kitengo cha CALL CENTER akitoa maelezo namna huduma
wanayotoa ikiwemo kupokea simu zaidi ya 200 kwa siku katika kituo hicho
ambapo wamefanikiwa kuwafikia watanzania mbalimbali
Kikao cha Maafisa Habari wa Wizara ya Afya na taasisi zake katika
kampeni maalum ya ‘Tumeboresha Sekta ya Afya’ inayolenga kueleza
mafanikio makubwa yaliyofikiwa katika kipindi cha miaka mitatu ya
Serikali ya awamu ya tano chini ya Rais Dkt. John Magufuli.
Na WAMJW, Dar es Salaam.
Mfuko
wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) umejivunia kuongeza wigo wa wanufaika
kwa kuwafikia Wananchi mbalimbali ikiwemo Wakulima kupitia vyama vyao
vya ushirika kwenye huduma ya Ushirika Afya na watoto kupitia huduma ya
Toto Afya Kadi. Mfuko pia umewezesha upatikanaji wa huduma za Madaktari
Bingwa katika mikoa ya pembezoni pamoja na kuwezesha upatikanaji wa
vifaa tiba vya kisasa katika Hospitali hapa nchini.
Hayo
yameelezwa na Meneja Uhusiano wa Mfuko huo Bi. Anjela Mziray wakati wa
ziara maalum ya Maafisa Habari wa Wizara ya Afya na taasisi zake katika
kampeni maalum ya ‘Tumeboresha Sekta ya Afya’ inayolenga kueleza
mafanikio makubwa yaliyofikiwa katika kipindi cha miaka mitatu ya
Serikali ya awamu ya tano chini ya Rais Dkt. John Magufuli.
Wakiwa
Makao Makuu ya NHIF, Maafisa hao waliweza kutembelea maeneo mbalimbali
ya Mfuko huo kujionea namna huduma zinazotolewa na Mfuko huo sambamba na
mafaniko waliyofikia katika sekta ya Afya.
Awali
akizungumza mambo mbalimbali Bi. Anjela Mziray aliwaeleza Maafisa hao
kuwa Serikali inakusudia kuwafikia wananchi wote na huduma bora za afya.
Katika kutekeleza hili Mfuko umewezesha Madaktari Bingwa wa magonjwa ya
mbalimbali kama ya Wanawake, watoto, moyo, macho, kinywa na pua na
mabingwa wa upasuaji kutoa huduma katika mikoa ya pembezoni kwa kipindi
maalum.
"Kwa ujumla watu
zaidi ya 20,289 wamefikiwa na huduma hii na kati ya hao watu 938
wamefanyiwa upasuaji wa kitalaam na hii ni katika mikoa ya Kigoma,
Katavi, Rukwa, Lindi, Mara, Manyara, Geita, Njombe na Ruvuma huku baadhi
ya mikoa tukienda mara mbili” alieleza Bi. Anjela Mziray.
Aidha,
katika mafaniko mengine ya kuboresha upatikanaji wa huduma, Mfuko
unashiriki juhudi za Serikali za uwekezaji katika viwanda. Mfuko kwa
kushirikiana na baadhi ya taasisi zingine unawekeza katika kiwanda cha
uzalishaji wa bidhaa za hospitali zitokanazo na malighafi ya pamba na
kiwanda hiko kitajengwa Bariadi Mkoani Simiyu huku kikitarajiwa
kuzalisha aina 24 za bidhaa hizo. Wadau wengine wanaoshiriki katika
uwekezaji huu ni pamoja na Serikali ya mkoa wa Simiyu, WCF, TFDA, TBS,
MSD, TIB, TIRDO na taasisi zingine.
Katika
jitihada za kuhakikisha wananchi wanapata huduma, alieleza kuwa Mfuko
kwa kushirikiana na Benki ya Maendeleo ya Ujerumani umenawezesha wamama
wajawazito kupata bima ya afya ili waweze kupata huduma katika
hospitali. Mpaka sasa wajawazito wapatao 1,044,000 wameshafikiwa na
mpango huu katika mikoa ya Tanga, Mbeya, Njombe, Lindi na Mtwara.
Mfuko
huo pia umeweza kurahisisha upatikanaji wa huduma kwa kutumia mifumo ya
Tehama inayowezesha kutambua wanachama katika vituo, kurahisisha
ulipaji wa madai ya watoa huduma kwa wakati, kurahisisha usajili wa
wanachama na kuharakisha utoaji wa vitambulisho.
Akizungumzia
hili Meneja wa Mifumo ya Tehama Bw. Bakari Yahaya alisema kwa sasa
mifumo inamwezesha mwanachama kupata ujumbe mfupi kwenye simu yake mara
tu kadi yake au ya mtegemezi wake inapotumika kwa matibabu.
Mfuko
huu sasa umefanikiwa kuwa na ofisi zake katika mikoa yote ikiwemo
Tanzania Bara na Zanzibar huku wakiboresha mfumo wa mawasiliano kwa
kuwa na kituo cha huduma kwa wateja kwa ajili ya kupokea simu za wadau
siku zote za juma bila malipo kwa wapigaji. Simu hiyo ni 0800 110063.
Akimalizia
maelezo yake alisema, Mfuko umefanikiwa kupata cheti cha ubora wa
huduma kwa viwango vya kimataifa ( ISO 9001:2015). "Katika hili
tunajivunia kuimarika kwa huduma na ufanisi katika utekelezaji majukumu
ya Mfuko kwa manufaa ya wadau wote wa Mfuko" alisema Bi. Mziray.
Mwisho.
0 on: "NHIF YAJIVUNIA KUONGEZA WIGO WAKUWAFIKIA WANANCHI"