Waziri wa Afya, Maendeleo ya jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu akitoa ufafanuzi wa jambo fulani mbele ya kamati ya kudumu ya Bunge ya huduma na maendeleo ya jamii, wakati akiwasilisha taarifa ya Wizara ya Afya, katika ukumbi wa Bunge wa Pius Msekwa jijini Dodoma.
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile akitoa ufafanuzi wa jambo fulani mbele ya kamati ya kudumu ya Bunge ya huduma na maendeleo ya jamii, wakati wa uwasilishwaji wa taarifa ya Wizara ya Afya, uliofanywa na Waziri wa Afya, Mhe. Ummy Mwalimu (hayupo kwenye picha) katika ukumbi wa Bunge wa Pius Msekwa jijini Dodoma.
Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Muhammad Bakar Kambi akielezea jambo mbele ya kamati ya kudumu ya Bunge ya huduma na maendeleo ya jamii, wakati wa uwasilishwaji wa taarifa ya Wizara ya Afya, uliofanywa na Waziri wa Afya, Mhe. Ummy Mwalimu katika ukumbi wa Bunge wa Pius Msekwa jijini Dodoma.
Mkurugenzi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili Prof. Laurence Museru akielezea jambo mbele ya kamati ya kudumu ya Bunge ya huduma na maendeleo ya jamii, wakati wa uwasilishwaji wa taarifa ya Wizara ya Afya katika ukumbi wa Bunge wa Pius Msekwa jijini Dodoma.
Mkurugenzi wa Taasisi ya Moyo (JKCI) Prof. Mohamed Janabi akielezea jambo mbele ya kamati ya kudumu ya Bunge ya huduma na maendeleo ya jamii, wakati wa uwasilishwaji wa taarifa ya Wizara ya Afya katika ukumbi wa Bunge wa Pius Msekwa jijini Dodoma.
Mkurugenzi wa Taasisi ya Mifupa MOI Dkt. Respicious Boniface akielezea jambo mbele ya kamati ya kudumu ya Bunge ya huduma na maendeleo ya jamii, wakati wa uwasilishwaji wa taarifa ya Wizara ya Afya katika ukumbi wa Bunge wa Pius Msekwa jijini Dodoma.
Baadhi ya Wakurugenzi kutoka Wizara ya Afya, na baadhi kutoka Taasisi za Wizara wakifuatilia kwa makini uwasilishwaji wa taarifa ya Wizara ya Afya, uliofanywa na Waziri wa Afya, Mhe. Ummy Mwalimu katika ukumbi wa Bunge wa Pius Msekwa jijini Dodoma.
Wajumbe wa ya kudumu ya Bunge ya huduma na maendeleo ya jamii, Wakurugenzi wa Wizara, na baadhi ya Taasisi zake, wakijadili taarifa ya utendaji ya Wizara ya Afya katika ukumbi wa Bunge wa Pius Msekwa jijini Dodoma.
JUMLA YA WAGONJWA 19 WAPANDIKIZWA FIGO NDANI YA MIEZI 5
Na WAMJW - DODOMA
WAZIRI wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu amesema kuwa katika kipindi cha Mwezi Julai 2018 hadi Desemba 2018 jumla ya wagonjwa 19 walipata huduma ya upandikizwaji wa figo, hivyo kufikisha jumla ya wagonjwa 28 waliopata huduma hii toka Hospitali ilivyoanza kutoa huduma za kupandikiza figo mwezi Novemba 2017.
Amesema hayo wakati akiwasilisha taarifa ya utendaji ya Wizara ya Afya mbele ya kamati ya kudumu ya Bunge ya huduma na maendeleo ya jamii, katika ukumbi wa Bunge wa Pius Msekwa jijini Dodoma.
Waziri Ummy amesema kuwa Serikali imeokoa jumla ya shilingi bilioni 2.24, ambazo zingetumika kupeleka wagonjwa 28 nje ya nchi kupata matibabu yakupandikizwa figo.
"Gharama ya huduma hii katika Hospitali ya Taifa Muhimbili ni kati ya shilingi milioni 20 mpaka 30 kwa mgonjwa mmoja wakati nje ya nchi gharama hii ni kati ya shilingi milioni 100 mpaka 120. Serikali imeokoa jumla ya shilingi bilioni 2.24 ambazo zingetumika kwaajili ya matibabu hayo nje ya nchi" Alisema Waziri Ummy.
Kwa upande mwingine Waziri Ummy amesema kuwa Hospitali ya Taifa Muhimbili iliona jumla ya wagonjwa 30,189, Idara ya Utengamano ilihudumia wagonjwa 22,379, huku Idara ya Madawa ilihudumia maombi ya dawa 519,216 na Kitengo cha Figo kilitoa huduma za kusafisha damu kwa mizunguko 13,248, huku Jumla ya wagonjwa mahututi 960 walihudumiwa katika ICU za Hospitali.
Mbali na hayo Waziri Ummy amesema kuwa Katika kipindi cha Mwezi Julai 2018 hadi Disemba 2018 Hospitali imetoa huduma za kupandikiza vifaa vya usikivu kwa watoto 11 na kufikisha jumla ya watoto 21 waliopata huduma hii toka ilipoanza mwezi Juni, 2017, jambo lililosaidia kuokoa zaidi ya shilingi milioni 840 ambazo zingetibu watoto 21.
"Kabla ya hapo huduma hii ilikuwa inapatikana nje ya nchi kwa gharama kati ya shilingi milioni 80 mpaka 100 kwa mtoto mmoja, huku Hospitali ya Taifa Muhimbili gharama nishilingi milioni 35 mpaka 40" alisema Waziri Ummy.
Wakati akijibu maswali ya Wabunge wa kamati hiyo Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile amesema kuwa Taasisi ya Moyo (JKCI) imeweza kufanya upasuaji kwa wagonjwa 211, kati ya wagonjwa waliofanyiwa upasuaji, watu wazima walikuwa 89 na watoto walikuwa 60, huku watu wazima 62 wenye matatizo kwenye mishipa ya damu walifanyiwa upasuaji wa mishipa ya damu.
Aidha, Dkt. Faustine Ndugulile amesema kuwa, wagonjwa 521 walipatiwa matibabu ya upasuaji wa moyo kupitia tundu dogo kwa upande wa mtambo maalum (catheterization laboratory).
Mwisho.
0 on: "JUMLA YA WAGONJWA 19 WAPANDIKIZWA FIGO NDANI YA MIEZI 5"