Waziri Ummy Mwalimu baada ya kutoa tamko la maadhimisho ya siku ya ukoma Duniani ambayo itafanyika kesho akiwakabidhi waathirika wa ukoma chakula kwenye makazi yaliyopo Nunge wilayani Kigamboni.Siku ya ukoma Kitaifa itafanyika kesho makazi ya watu waishio na ukoma Wilayani Mvomero Mkoani Morogoro.
Tanzania ilifikia viwango vya utokomezaji wa Ukoma kitaifa mnamo mwaka 2006 kwa kiwango cha chini ya mgonjwa 1 kati ya watu 10,000 lakini Ukoma bado unaendelea kuwa tatizo la kiafya miongoni mwa jamii nchini kwetu.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu amesema hayo leo katika Tamko lake la leo alilolitoa mbele ya vyombo vya habari kuhusu hali ya Ukoma Nchini katika Makao ya Wazee Nunge Kigamboni Jijini Dar es Salaam.
Waziri Mwalimu amesema kuwa kwa mujibu wa takwimu za Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Kifua kikuu na Ukoma (NTLP) za mwaka 2017, jumla ya wagonjwa wapya 1,933 waligunduliwa na hivyo kufanya kiwango cha ugunduzi kuwa watu 4 kwa kila watu 100,000.
Aidha ameongeza kuwa takwimu hizi zinaifanya Tanzania kuendelea kuwa miongoni mwa nchi 22 zenye wagonjwa wengi wa Ukoma duniani nchi nyingien ni pamoja na India, Indonesia, Brazil, Ethiopia, Msumbiji, Nigeria na DRC Kongo.
‘’Hivi sasa bado kuna mikoa kumi ambayo inagundua wagonjwa wapya wa Ukoma wengi zaidi kila mwaka na kuchangia karibia 80% ya wagonjwa wote. Mikoa hiyo ni pamoja na: Lindi, Rukwa, Mtwara, Morogoro, Pwani; Tanga, Geita, Dodoma, Tabora na Kigoma’’ Alongeza Waziri Ummy.
Amezitaja Wilaya zenye kiwango kikubwa cha ugonjwa wa ukoma kuwa ni 20 ambazo kiwango cha ukubwa wa tatizo la Ukoma lipo juu sana na bado hazijafikia lengo la utokomezaji, nazo ni amabazo ni Liwale, Lindi vijijini, Nachingwea, Ruangwa, Nanyumbu, Masasi mjini, Pangani, Mkinga, Korogwe, Mvomero, Kilombero, Morogoro vijijini, Ulanga, Shinyanga manispaa, Mafia, Rufiji, Kilwa, Chato, Nkasi, na Mpanda.
Waziri Ummy aidha amesema Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto kwa kushirikiana na Wizara ya TAMISEMI zimendelea kuhakikisha Ukoma unatokomezwa kabisa kwa Kuhakikisha dawa za kutibu Ukoma zinaendelea kupatikana wakati wote na bila malipo yoyote.
Amezitaja juhudi nyingine kuwa ni kuendesha kampeni za uibuaji wa wagonjwa wapya ngazi ya jamii kwa kuwashirikisha watoa huduma ngazi ya jamii (Leprosy Elimination Campaigns) hasa katika wilaya zenye kiwango kikubwa cha wagonjwa wa Ukoma.
Amesema pamoja na hatua zinazochukuliwa na serikali na mafanikio zipo changamoto kubwa mbili ambazo ni jamii kuendelea kushikilia imani potofu juu ya Ukoma kuwa ni ugonjwa wa kurithi au kulogwa na wagonjwa kuchelewa kujitokeza kupata matibabu hadi wanapopata ulemavu.
‘’Natoa rai kwa jamii, wazazi na walezi kuwa sote tujenge tabia ya kuchunguza miili yetu na ya watoto wetu na endapo utaona mojawapo ya dalili za Ukoma ambazo ni baka au mabaka mwilini yenye rangi ya shaba na hayana hisia, vijinudu kwenye ngozi au mishipa ya fahamu kuvimba. Dalili nyingine ni ganzi kwenye mikono na miguu. Unashauriwa kwenda kwenye kituo cha tiba kilicho karibu nawe kwa uchunguzi bila kuchelewa’’. Alisisitiza Mwalimu.
Ameongeza kuwa kupima afya kutawawezesha wataalam wa afya kuchunguza na kubainisha kama mgonjwa ana Ukoma ili apate tiba sahihi mapema na hivyo kuzuia maambukizi na ulemavu wa kudumu unaoweza kuzuilika uku akitaka jamii kifahamu kuwa ugonjwa wa Ukoma unatibika.
Siku ya Ukoma Duniani huadhimishwa ulimwenguni kote kila Jumapili ya mwisho ya mwezi Januari. Kwa mwaka huu, siku hii itaadhimishwa tarehe 27 Januari,2019.Hapa Tanzania maadhimisho haya kitaifa yatafanyika wilayani Mvomero,Mkoani Morogoro. |
0 on: "JUMLA YA WAGONJWA WAPYA 1,933 WALIGUNDULIWA NA UKOMA NCHINI"