Serikali kupitia Wizara ya Afya,
Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imebainisha maeneo muhimu
yaliyowekewa kipaumbele katika bajeti ili kuboresha miundombinu na hali ya
upatikanaji wa Huduma za afya nchini.
Akieleza taarifa ya utekelezaji wa
bajeti ya wizara kwa kipindi cha nusu mwaka kuanzia Julai hadi Desemba 2018 mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya
Jamii jana jijini Dodoma. Waziri wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,
Wazee Mh. Ummy Mwalimu amesema wizara hiyo iliidhinishiwa na Bunge kupokea na kutumia bajeti ya jumla ya
shilingi 866,233,475,000 ambapo Kati ya fedha hizo kiasi cha shilingi 304,473,476,000 ilikua ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida
ambapo shilingi 88,465,756,000 ni kwa ajili ya matumizi mengineyo na shilingi 216,007,720,000
kwa ajili ya Mishahara ya watumishi walio makao makuu ya Wizara pamoja na
Watumishi wa Taasisi zilizo chini ya Wizara.
Waziri Ummy amesema fedha zilizopokelewa katika
kipindi cha Julai hadi Desemba 2018 zimeainishwa katika utekelezaji wa majukumu ya wizara katika kipindi hicho ambapo
maeneo muhimu kama Chanjo, afya ya mzazi na mtoto, mapambano dhidi ya VVU na
UKIMWI, upatikanaji wa dawa, vifaa na vifaa tiba, upatikanaji wa damu salama,
uimarishaji wa huduma za kibingwa, Utoaji
wa huduma za Afya katika Hospitali za Kanda, Maalum, Hospitali ya Taifa ya Muhimbili
na Hospitali za Rufaa za Mikoa pamoja na uhakiki ubora wa huduma za afya
yalipewa kipaumbele.
Aidha, Waziri Ummy amesema Wizara imeendelea kusimamia na
kuratibu shughuli zilizokuwa zimepangwa kutekelezwa na Taasisi zilizopo chini
yake. Taasisi hizo ni pamoja na Bohari Kuu ya Dawa (MSD), Mfuko wa Taifa wa
Bima ya Afya (NHIF), Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA), Taasisi ya Chakula na
Lishe (TFNC), Wakala wa Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA), Taasisi ya
Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR) na Mabaraza ya Kitaaluma.
Hata hivyo, pamoja na mafanikio mbalimbali yaliyopatikana
katika utekelezaji wa Majukumu ya Wizara (Idara Kuu ya Afya), Waziri Ummy
amebainisha changamoto mbalimbali zikiwemo
Vituo vya
kutolea huduma za Afya kutowasilisha mahitaji ya dawa, Vifaa, Vifaa tiba na
Vitendanishi kwa wakati, Upatikanaji wa Huduma Bora na za Uhakika za
Uzazi, Mama na Mtoto,
Upungufu wa watumishi wenye taaluma ya kutoa
huduma za afya ikilinganishwa na mahitaji, Wigo mdogo wa wananchi walio katika mifumo ya Bima za
Afya pamoja na Kuongezeka kwa watu wenye magonjwa yasiyo ya
kuambukiza.
0 on: "SERIKALI YABAINISHA VIPAUMBELE MUHIMU KATIKA KUBORESHA HUDUMA ZA AFYA NCHINI"