Like us on Facebook

Inaendeshwa na Blogger.

Tafuta katika Blogu Hii

Kumbukumbu la Blogu

Instagram

visitors

display number of visitors

Popular Posts

Pages

Flickr Images

Jumatatu, 28 Januari 2019

UKOMA HAUNA UHUSIANO NA IMANI ZA KISHIRIKINA - SERIKALI

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile (kushoto) akitoa kingatiba kwa mtoto aliyekuwa akiishi na mgonjwa wa ukoma. Kingtiba hiyo itamlinda dhidi ya ugonjwa wa ukoma imezinduliwa na Dkt. Ndugulile katika maadhimisho ya siku ya Ukoma Duniani yaliyofanyika Wilayani Mvomero, Morogoro.

Baadhi ya Wanafunzi waliofika kusikiliza ujumbe kuhusu Ugonjwa wa Ukoma na kupata Kingatiba ya kuzuia ugonjwa huo ilikuwa ikitolewa katika viwanja vya kijiji cha Chazi, vilivyopo Wilaya ya Mvomero Mkoa wa Morogoro.

Wazee waliopata msaaada wa viatu vya kutembelea toka Taasisi ya GLRA inayowasaidai watu wenye ugonjwa wa ukoma nchini, wakifuatilia kwa makini, ujumbe kutoka kwa mgeni rasmi  Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile katika siku ya Ukoma Duniani.

Wakina mama wa Kijiji cha Chazi, Mvomero , Mkoa wa Morogoro wakifuatilia kwa makini, ujumbe kutoka kwa mgeni rasmi  Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile katika siku ya Ukoma Duniani.

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile (Wapili kushoto) akifuatilia kwa makini risala kutoka kwa Mwakilishi wa Wazee wenye ulemavu wanaoishi na Ukoma katika kijiji cha Chazi, Wilaya ya Mvomero Mkoani Morogoro

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile (kulia)akisalimiana na Mzee Anthony Martin (kushoto) wakati alipotembelea makazi ya wasiojiweza ya Chazi, Katika Wilaya ya Mvomero Mkoani Morogoro

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile akishika kito cha Mtumbwi katika moja kati ya banda la maonesho katika kijiji cha Chazi, Wilaya ya Mvomero Mkoani Morogoro

Picha ya pamoja, Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulike (wa nne kutoka kushoto, walioketi) akiwa na wadau wa Sekta ya Afya nchini.UKOMA HAUNA UHUSIANO NA IMANI ZA KISHIRIKINA - SERIKALI

Na WAMJW -Mvomero, Morogoro.

“Ugonjwa wa ukoma hausababishwi na imani za kishirika bali ni vimelea vya magonjwa ambavyo huingia ndani ya mwili na kusababisha ukoma”

Hiyo ni kauli ya Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile alipokuwa akizungumza na waathirika wa ugonjwa wa ukoma pamoja na wananchi katika maadhimisho ya siku ya Ukoma Duniani, wilayani Mvomero, katika Mkoa waMorogoro.

 Dkt. Ndugulile amewaasa wananchi kuachana na imani za kishirikina  kwa kuamini kuwa ya kwamba ugonjwa huo unahusika moja kwa moja na imani hizo za giza.

“Dhana ya kwamba ugonjwa huu ni wa kurogwa siyo kweli, ugonjwa wa ukoma hausababishwi na mtu kulogwa wala kutupiwa jini bali ni vimelea ambavyo huingia mwilini na kusababisha ugonjwa wa ukoma, ni watu kama mimi na wewe” anasema Dkt Ndugulile.

Aidha Dkt Ndugulile ametumia nafasi hiyo kuwaelimisha wananchi kuwa ugonjwa wa ukoma unatibika na kusema kuwa dawa za kutibu ugonjwa huo zipo na kuwaondolea hofu ya kuwa ugonjwa huo kutotibika. Hata hivyo Dkt. Ndugulile ametoa rai kwa wananchi wote kujitokeza mapema katika vituo vya kutolea huduma za afya kupata huduma za matibabu pindi wanapohisi kuwa na dalili za ugonjwa wa ukoma.

“Mtu yeyote ambaye anaanza kuona mabadiliko kwenye ngozi yake, anapata mabaka ambayo hayaelewi au kupoteza hisia pindi unapojigusa ni muda wa kwenda hospitalini kufanya uchunguzi na kama utagundulika kuwa na vimelea vya ugonjwa wa ukoma utapewa matibabu” alisisitiza Dkt. Ndugulile.

Dkt. Ndugulile amewataka wananchi kuwa mabalozi wa kuwaelimisha watu wengine juu ya dalili na athari za ugonjwa wa ukoma. “Niwaombe ndugu wananchi tuendelee kutoa elimu kuhusiana na ugonjwa huu ni ugonjwa ambao tunaweza tukauzuia na tusiwe na athari kwenye jamii na tusingependa kuona kwenye zama hizi watu wanapata athari za kudumu na wanapoteza viungo, hisia katika sehemu za miili yao au kuharibika ngozi kwa sababu ya kutopata matibabu mapema” alifafanua Dkt Ndugulile.

Naibu Waziri huyo wa Afya amesema kuwa Serikali ipo katika hatua nzuri za kutokomeza ugonjwa wa ukoma nchini licha ya changamoto ambazo zipo katika baadhi ya maeneo sugu ambayo ugonjwa huo umeonekana kuwa ni tatizo. “Takwimu zinaonyesha kuwa takribani watu 1993 huugua ugonjwa wa ukoma kila mwaka huku mikoa ya Lindi, Rukwa, Mtwara, Pwani, Tanga, Geita, Dodoma, Tabora, Kigoma na Mkoa wa Morogoro ikiwa na idadi kubwa ya wagonjwa” alisema Dkt. Ndugulile.

Sasa hivi tumepiga hatua kubwa, tunajua jinsi gani ugonjwa unaambukizwa, na namna ya kuutibu pamoja na kujikinga dhidi ya maambukizi mapya, naamini kwa mikakati iliyopo tunaweza kuutokomeza ugonjwa huu.

Akizungumiza mikakati iliyopo Dkt Ndugulile amesema kuwa pamoja na elimu ambayo wamekuwa wakiitoa, Serikali imehamishia nguvu kwenda kwenye jamii moja kwa moja kuwabaini wagonjwa wa ukoma. “Hatusubiri watu watufate, tumewekeza nguvu nyingi kwenye jamii na kuwafikia huko huko maeneo wanayoishi” alisema Dkt Ndugulile.

Kwa upande mwingine, Dkt Ndugulile amezindua Mpango wa Kingatiba ya Ugonjwa wa Ukoma mahususi kwa wale ambao wamekuwa wakiishi na wagonjwa wa ukoma ili waweze kujikinga kutopata ugonjwa huo na kutoa rai kwa wananchi wote ambao wamekuwa wakiishi na wagonjwa wa ukoma kujitokeza katika vituo vya huduma za afya kumeza dawa hizo za kujikinga na ukoma.

“Mtu mwenye ukoma na ambaye amekunywa dawa za kingatiba hawezi kusambaza ugonjwa huu na tunaweza kuishi na kushirikiana naye kufanya shughuli mbalimbali kimaendeleo” alisema Dkt Ndugulile na kuwaasa wananchi kuacha tabia za kuwanyanyapaa wenye ukoma.

Dkt Ndugulile ameipongeza taasisi ya GLRA kutoka Ujerumani inayojihusisha na kuwatunza watu wenye ukoma kwa kuwaanzishia miradi ya ujasiriamali na kuwaunganisha wahanga wa ugonjwa huo na jamii pamoja na kuwapongeza pia wagonjwa wa ukoma kujishughulisha na shughuli za uzalishaji kipato kuliko kuwa omba omba barabarani.

Awali akitoa salamu zake Rais wa Taasisi ya GLRA Bw. Patric Meisen amesema kuwa anafuraha kuona Tanzania na Ujerumani zikiwa na mahusiano mazuri na kuahidi kuendelea kuwasaida waathirika wa ugonjwa ukoma nchini.

“Tumekuwa tukifanya kazi na wataalam wa afya katika kuwatunza waathirika waugonjwa wa ukoma, hatujaishia hapo tuu, tumewasaidia waathirika wa ugonjwa huu kwa kuwapatia mitaji itakayowasaidia kujiongezea kipato ambacho kitawasaidia” alisema Bw. Meisen.

Siku ya Ukoma Duniani huadhimishiwa kila jumapili ya mwisho wa mwezi Januari, ambapo kwa mwaka huu 2019, maadhimisho hayo kitaifa yamefanyika Wilayani Mvomero, Mkoa wa Morogoro yakiwahusisha wadau mbalimbali wa Sekta ya afya huku kauli mbiu ikiwa ni *“Tutokomeze Ubaguzi, Unyanyapaa na Chuki dhidi ya Waathirika wa Ukoma”*

Mwisho

0 on: " UKOMA HAUNA UHUSIANO NA IMANI ZA KISHIRIKINA - SERIKALI"