TAMKO
LA MHE. UMMY MWALIMU (MB) WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA,
WAZEE NA WATOTO KATIKA KUADHIMISHA SIKU YA UKOMA DUNIANI TAREHE
27/01/2019
KIGAMBONI, DAR ES SALAAM
Ndugu wanahabari,
Siku
ya Ukoma Duniani huadhimishwa ulimwenguni kote kila Jumapili ya mwisho
ya mwezi Januari. Kwa mwaka huu, siku hii itaadhimishwa tarehe 27
Januari, 2019.
Lengo kuu
la maadhimisho haya ni kukumbusha umma wa watanzania juu ya ugonjwa
huu. Ni dhahiri kuwa ugonjwa wa Ukoma umekuwa ukiogopwa sana katika
jamii yetu toka enzi na enzi hasa kutokana na ukweli kwamba unasababisha
ulemavu wa kudumu mwilini na kufanya waathirika kuwa tegemezi na
kutothaminiwa.
Sanjali na
madhimisho haya, hapa Tanzania tunaadhimisha miaka 60 ya uwepo wa
Shirika la Ujerumani linaloshughulikia masuala ya Kifua kikuu na Ukoma
(GLRA). Shirika hili limekuwa mstari wa mbele katika kuisaidia serikali
kuhakikisha Ukoma unatokomezwa kwa kufadhili shughuli mbali mbali ikiwa
ni pamoja na kutoa vyombo vya usafiri kwa waratibu wa Kifua kikuu na
Ukoma nchi nzima.
Ndugu wanahabari,
Siku
ya Ukoma Duniani inatupa fursa ya kutathmini mwelekeo wa jitihada zetu
nchini na zile za kimataifa katika kupambana na ugonjwa huu. Kauli mbiu
katika maadhimisho ya mwaka huu ni “TUTOKOMEZE UBAGUZI, UNYANYAPAA NA
CHUKI DHIDI YA WAATHIRIKA WA UKOMA”. Ni kweli kuwa waathirika wengi wa
Ukoma wananyanyapaliwa na kubaguliwa katika maeneo mengi, takriban
asilimia 50 ya wagonjwa wa Ukoma hupatwa na sonona na huishi maisha ya
huzuni na wasi wasi mkubwa. Haya yote husababishwa na mtazamo hasi wa
jamii dhidi ya waathirika wa ugonjwa wa Ukoma. Mtazamo huu hasi ndio
kikwazo kikubwa katika vita ya kutokomeza Ukoma duniani na hapa nchini.
Serikali,
wadau na wananchi wote wanahimizwa kuungana na kuongeza nguvu katika
kupinga matukio vyote vya ubaguzi na unyanyapaa ikiwa ni pamoja na
kuhakikisha hakuna sheria kandamizi kwa watu walioathirika na ugonjwa wa
Ukoma. Kwa kufanya kazi pamoja na kupinga kwa nguvu zote vitendo hivi
itatusaidia kupiga hatua mbele kuelekea kutokomeza Ukoma.
Ndugu wanahabari,
Pamoja
na kwamba nchi yetu ilifikia viwango vya utokomezaji wa Ukoma kitaifa
mnamo mwaka 2006 kwa kiwango cha chini ya mgonjwa 1 kati ya watu 10,000,
Ukoma bado unaendelea kuwa tatizo la kiafya miongoni mwa jamii nchini
kwetu. Kwa mujibu wa takwimu za Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Kifua kikuu
na Ukoma (NTLP) za mwaka 2017, jumla ya wagonjwa wapya 1,933
waligunduliwa na hivyo kufanya kiwango cha ugunduzi kuwa watu 4 kwa kila
watu 100,000. Takwimu hizi zinaifanya Tanzania kuendelea kuwa miongoni
mwa nchi 22 zenye wagonjwa wengi wa Ukoma duniani nchi nyingien ni
pamoja na India, Indonesia, Brazil, Ethiopia, Msumbiji, Nigeria na DRC
Kongo. Hivi sasa bado kuna mikoa kumi ambayo inagundua wagonjwa wapya wa
Ukoma wengi zaidi kila mwaka na kuchangia karibia 80% ya wagonjwa wote.
Mikoa hiyo ni pamoja na: Lindi, Rukwa, Mtwara, Morogoro, Pwani; Tanga,
Geita, Dodoma, Tabora na Kigoma.
Aidha,
bado zipo wilaya 20 ambazo kiwango cha ukubwa wa tatizo la Ukoma lipo
juu sana na bado hazijafikia lengo la utokomezaji, nazo ni Liwale,
Lindi vijijini, Nachingwea, Ruangwa, Nanyumbu, Masasi mjini, Pangani,
Mkinga, Korogwe, Mvomero, Kilombero, Morogoro vijijini, Ulanga,
Shinyanga manispaa, Mafia, Rufiji, Kilwa, Chato, Nkasi, na Mpanda.
Ndugu wanahabari,
Wizara
ya Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto kwa kushirikiana na
Wizara ya TAMISEMI inatekeleza shughuli mbali mbali katika kuhakikisha
Ukoma unatokomezwa kabisa. Shughuli hizo ni pamoja na :
Kuhakikisha dawa za kutibu Ukoma zinaendelea kupatikana wakati wote na bila malipo yoyote,
Kuendesha
kampeni za uibuaji wa wagonjwa wapya ngazi ya jamii kwa kuwashirikisha
watoa huduma ngazi ya jamii ( Leprosy Elimination Campaigns) hasa katika
wilaya zenye kiwango kikubwa cha wagonjwa wa Ukoma,
Kuendelea
kutoa elimu kwa jamii kuhusu dalili za Ukoma na upatikanaji wa huduma
kwa kutumia vifaa vya habari, Elimu na mawasiliano kama vile
vipeperushi, mabango na mikanda ya video,
Utekelezaji
wa shughuli za kuzuia ulemavu unaotokana na Ukoma ikiwemo kutathmini
wagonjwa wenye vidonda, kufanya upasuaji maalum, huduma za kitaalam za
macho na utoaji wa viungo bandia pamoja na viatu maalum.
Ndugu wanahabari,
Pamoja
na hatua zinazochukuliwa na serikali na mafanikio zipo changamoto kubwa
mbili ambazo ni jamii kuendelea kushikilia imani potofu juu ya Ukoma
kuwa ni ugonjwa wa kurithi au kulogwa; na wagonjwa kuchelewa kujitokeza
kupata matibabu hadi wanapopata ulemavu. Ukoma ni ugonjwa wa kuambukizwa
unaosababishwa na vimelea vinavyoshambulia mishipa ya fahamu na
huambukizwa kwa njia ya hewa pekee.
Nitoe
rai kwa jamii, wazazi na walezi kuwa sote tujenge tabia ya kuchunguza
miili yetu na ya watoto wetu. Endapo utaona mojawapo ya dalili za Ukoma
ambazo ni baka au mabaka mwilini yenye rangi ya shaba na hayana hisia,
vijinudu kwenye ngozi au mishipa ya fahamu kuvimba. Dalili nyingine ni
ganzi kwenye mikono na miguu. Unashauriwa kwenda kwenye kituo cha tiba
kilicho karibu nawe kwa uchunguzi bila kuchelewa. Hii itawawezesha
wataalam wa afya kuchunguza na kubainisha kama mgonjwa ana Ukoma ili
apate tiba sahihi mapema na hivyo kuzuia maambukizi na ulemavu wa kudumu
unaoweza kuzuilika.
Ugonjwa
wa Ukoma unatibika. Mgonjwa aliyeanza tiba hawezi kuambukiza mtu
mwingine na hivyo hakuna sababu ya kumtenga na anaweza kuendelea na
shughuli za kawaida za maisha.
Tiba ya Ukoma inapatikana nchini kote na hutolewa bila malipo kwa wagonjwa wote.
Nirudie
tena kuwa, pale tunapoona mabadiliko yoyote yanajitokeza kwemye miili
yetu twende mapema katika vituo vyetu vya huduma kuchunguzwa ili tupate
matibabu stahili.
Ndugu wanahabari,
Aidha,
napenda kuwashukuru watoa huduma katika vituo vya huduma za afya kote
nchini kwa juhudi wanazofanya kila siku kuhakikisha ugonjwa huu si
tatizo la kiafya tena nchini. Pia wanahabari kwa kuendelea kuendelea
kuelimisha jamii kuhusu magonjwa mbalimbali.
Pia
nachukua nafasi hii kwa niaba ya serikali ya awamu ya tano ya Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli
kuyashukuru mashirika mbali mbali ya ndani na nje yanayounga mkono
juhudi zetu za kutokomeza Ukoma nchini kama vile Norvatis Foundation ya
Uswisi, Germany Leprosy and Tuberculosis Relief Association (GLRA) ya
Ujerumani, Nippon Foundation chini ya Sasakawa Memorial Health
Initiative ya Japani na Shirika la Afya Duniani (WHO) kwa michango yao
ya hali na mali katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa Ukoma hapa nchini
Tanzania.
“TUTOKOMEZE UBAGUZI, UNYANYAPAA NA CHUKI DHIDI YA WAATHIRIKA WA UKOMA”.
Asanteni kwa kunisikiliza!
0 on: "TAMKO LA MHE. UMMY MWALIMU (MB) KATIKA KUADHIMISHA SIKU YA UKOMA DUNIANI"