Like us on Facebook

Inaendeshwa na Blogger.

Tafuta katika Blogu Hii

Kumbukumbu la Blogu

Instagram

visitors

display number of visitors

Popular Posts

Pages

Flickr Images

Alhamisi, 30 Novemba 2017

WANAUME WAWE KIPAUMBELE KUPIMA VVU.

Naibu Waziri wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto dkt. Faustine Ndugulile akisisitiza jambo mbele ya Wadau na Watumishi wa Sekta ya Afya katika siku ya uzinduzi wa Mwongozo wa kutoa cheti kwa  maeneo ya kufanyia vipimo vya VVU  katika vituo vya kutolea huduma za Afya.

 Wadau wa masuala ya Afya wakifuatilia kwa ukaribu taarifa is juu ya Uzinduzi wa Mwongozo wa kutoa cheti kwa  maeneo ya kufanyia vipimo vya VVU  katika vituo vya kutolea huduma za Afya, tukio lililofanyika katika ofisi za NIMR jijini Da es salaam.

 Mkurugenzi wa Idara ya Uhakiki Ubora  toka Wizara ya afya Dkt. Mohamed Mohamed  akimkaribisha mgeni rasmi mapema leo katika siku ya Uzinduzi wa Mwongozo wa kutoa cheti kwa  maeneo ya kufanyia vipimo vya VVU  katika vituo vya kutolea huduma za Afya. 

 Mkurugenzi wa Idara ya Uhakiki Ubora  toka Wizara ya afya Dkt. Mohamed Mohamed (Wakwanza) akiteta jambo na Naibu Waziri wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto dkt. Faustine Ndugulile katika siku ya uzinduzi wa Mwongozo wa kutoa cheti kwa  maeneo ya kufanyia vipimo vya VVU  katika vituo vya kutolea huduma za Afya.

Mwakilishi kutoka CDC Kevin De Cock akiwasilisha salamu kutoka CDC mbele ya Naibu Waziri wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto dkt. Faustine Ndugulile (wakwanza kushoto) katika uzinduzi wa Mwongozo wa kutoa cheti kwa  maeneo ya kufanyia vipimo vya VVU  katika vituo vya kutolea huduma za Afya.

Mratibu Huduma ya Upimaji maambukizi ya VVU Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Ukimwi Peris Urasa akiwasilisha taarifa mbele ya mgeni rasmi (Hayupo kwenye picha) na wadau wa Afya katika kikao cha Uzinduzi wa Mwongozo wa kutoa cheti kwa  maeneo ya kufanyia vipimo vya VVU  katika vituo vya kutolea huduma za Afya.

 Mkurugenzi wa Mradi wa mtandao wa Afya Donan Mbando akimkabidhi Kitabu cha Mwongozo Naibu Waziri wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto dkt. Faustine Ndugulile  katika siku ya uzinduzi wa Mwongozo wa kutoa cheti kwa  maeneo ya kufanyia vipimo vya VVU  katika vituo vya kutolea huduma za Afya, wakwanza kushoto ni Mkurugenzi wa Idara ya Uhakiki Ubora  toka Wizara ya afya Dkt. Mohamed Mohamed.


 Picha ya pamoja ikiongozwa na Naibu Waziri wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto dkt. Faustine Ndugulile katika siku ya uzinduzi wa Mwongozo wa kutoa cheti kwa  maeneo ya kufanyia vipimo vya VVU  katika vituo vya kutolea huduma za Afya, tukio lililofanyika katika ofisi za NMRI jijini Da es salaam.






Na WAMJW-Dsm.
WANAUME  nchini wamesisitizwa kuwa kipaumbele katika kupima Maambukizi ya virus vya ukimwi (VVU) ili kusaidia juhudi za Serikali katika kupambana na vita dhidi ya maambukizo ya ukimwi.
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia ,Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile wakati wa uzinduzi wa Kiunzi kazi wa Kutoa cheti kwa maeneo ya kufanyia vipimo vya VVU katika vituo vya kutolea huduma za afya.
“ Wanaume tumekuwa wagumu sana katika kupima maambukizi ya virusi vya ukimwi na tukikutwa tuna maambukizi tunatakiwa tuanze kutumia dawa za kufubaza  kuliko kuwasubiri wenza wetu kwenda kupima na sisi ndo tupate majibu yetu kupitia wao” alisema Dkt. Ndugulile.
Aidha Dkt. Ndugulile amesema kuwa katika kuhakikisha inapamabana na UKIMWI  wameweka taratibu ya kila mwananchi anayepima maambukizi ya Ukimwi na akagundulika kuwa na virusi hivyo anaanza dawa za kufubaisha mara moja.
Kwa mujibu wake Dkt. Ndugulile amesema kuwa mpaka kufikia 2020 Serikali inataka kufikia malengo ya kimkakati ya 90 90 90 ambayo 90 ya kwanza inamaanisha watu wapime VVU  kufikia asilimia 90, 90 ya pili inamaanisha wanaopima VVU kama wana maambukizi waanze kutumia dawa za kufubaza na 90 ya tatu inamaanisha wenye VVU wawe wamefubaza ugonjwa huo.
Aidha Dkt. Ndugulile ametoa rai kwa Watanzania wote kuchangia mfuko wa Udhamini wa kupamabana na Maambukizi ya Ukimwi kwa kupitia namba 0684909090 ili mradi kuweza kuongeza rasirimali fedha zitakazosaidia kwenye mapambano hayo.
Mbali na hayo Dkt. Ndugulile amesema kuwa katika kuelekea maadhimisho ya Siku ya ukimwi Duniani ambayo huadhimishwa Decemba 1 kila mwaka watu wote wajitokeze kupima VVU.


Jumatatu, 27 Novemba 2017

HOTUBA YA MHE. DR FAUSTINE NDUGULILE (MB)






HOTUBA YA MHE. DR FAUSTINE NDUGULILE (MB) NAIBU WAZIRI WA AFYA MAENDELEO YA JAMII JINSIA WAZEE NA WATOTO KATIKA MKUTANO WA MWAKA WA MPANGO WA TAIFA WA KUDHIBITI KIFUA KIKUU NA UKOMA TAREHE 27 NOV -1 DISEMBA, 2017 MKOANI DODOMA

Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Muhammad Bakari Kambi,
Mkurugenzi wa Kinga Dkt. Neema Rusibamayila,
Naibu Meneja Mpango, Dkt. Liberate Mleoh,
Wadau wa Maendeleo kutoka mashirika mbali mbali ya kitaifa na kimataifa,
Waratibu wa Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Kifua Kikuu na Ukoma ngazi ya Taifa,
Waratibu wa  Kifua kikuu na Ukoma wa Mikoa na wilaya
Wageni wetu waalikwa.
Mabibi na Mabwana
Awali ya yote napenda niwapongeze kwa juhudi zenu za dhati kabisa katika kutekeleza majukumu yenu ili kuhakikisha kuwa magonjwa ya kifua kikuu na ukoma yanadhibitiwa na kuwa si tatizo la kiafya kwa watanzania.
Kama mnavyofahamu tatizo la kifua kikuu katika nchi yetu ni kubwa.  Kwa mujibu wa ripoti ya Shirika la Afya Duniani (WHO) ya kifua kikuu ya mwaka 2017, Tanzania ni miongoni mwa nchi 30 duniani zenye kiwango kikubwa cha ugonjwa wa Kifua kikuu. Inakadiriwa kuwa katika kila watanzania laki moja (100,000) watu mia mbili themanini na saba (287) wanaugua kifua kikuu kwa mwaka. Utafiti wa kutathmini ukubwa wa tatizo la Kifua kikuu nchini uliofanyika mwaka 2012/13 ulibaini kuwa kifua kikuu bado ni tatizo kubwa katika maeneo ya vijijini na kwa wazee wenye umri zaidi ya miaka 60.
Vile vile, kutokana na ripoti ya kifua kikuu ya Shirika la Afya Duniani ya mwaka 2017, Tanzania inakadiriwa kuwa na asilimia 1.3 ya wagonjwa wapya na asilimia 6.2 ya wagonjwa waliokwishatumia dawa za Kifua kikuu wana Kifua kikuu sugu. Takwimu hizi zinaweka makadirio ya kuwepo wagonjwa 830 wa kifua kikuu sugu kwa mwaka 2016. Maambukizi mseto ya Kifua kikuu na UKIMWI ni tatizo kubwa nchini ambapo asilimia 34 ya wagonjwa wa kifua kikuu wana maambukizi ya VVU na asilimia 91 ya wagonjwa hao walianzishiwa dawa za kufubaza VVU (ARV).
Kwa upande wa ugonjwa wa ukoma ni wazi kuwa ukubwa wa tatizo la ukoma unaendelea kupungua. Kwa mujibu wa takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) za mwaka 2016 inaonyesha kuwa tuna chini ya mgonjwa mmoja (0.4) katika kila watu 10,000.

Ndugu washiriki,
Miongoni mwa mafanikio katika mapambano dhidi ya kifua kikuu nchini ni kuwa wagonjwa wote wanaoanzishiwa matibabu, asilimia 90 wanapona kabisa, na asilimia 78 kati ya hao wanapatiwa matibabu katika ngazi ya jamii. Vile vile asilimia 71 ya wagonjwa wa Kifua kikuu sugu wanatibiwa na kupona kabisa.
Hata hivyo changamoto kubwa tuliyonayo hapa nchini ni kuweza kuwaibua wagonjwa wote wa Kifua kikuu cha kawaida na Kifua kikuu sugu ambapo kwa takwimu za sasa zinaonyesha kuwa tunashindwa kuwafikia wagonjwa takriban 85,000 wa Kifua kikuu na 600 wa Kifua kikuu sugu kwa mwaka. Vile vile mpaka sasa tumekwishagundua wagonjwa wawili wa kifua kikuu sugu zaidi (XDR-TB) kwa miaka ya 2014 (ameshapona kabisa) na 2017 yuko kwenye matibabu.

NdugU Washiriki
Wizara kupitia Mpango inatekeleza Mpango Mkakati wa miaka mitano wa Kudhibiti Kifua kikuu na Ukoma (2015-2020). Mikakati iliyowekwa ili kukabiliana nazo ni pamoja na:-
·        Kuhakikisha dawa za kutibu Kifua kikuu zinaendelea kupatikana wakati wote na bila malipo yoyote
·        Kuimarisha uwezo wa vituo vya ugunduzi wa Kifua kikuu  kwa kutumia teknolojia mpya ya vipimo kwa kutumia vinasaba vya GeneXpert MTB/RIF,
·        Kuimarisha uwezo wa maabara za kikanda zilizopo Dodoma, (Dodoma Hospitali) Mwanza, (Bugando) Mbeya (Mbeya Rufaa) na Kilimanjaro (Kibong’oto),
·        Kushirikisha sekta binafsi katika mapambano dhidi ya Kifua kikuu ikiwemo maduka ya dawa muhimu, famasi na hospitali binafsi katika kuibua wagonjwa wa Kifua kikuu,
·        Kuimarisha mikakati ya uibuaji wagonjwa wa Kifua kikuu kutoka kwa wachimbaji wadogo wadogo wa madini na jamii zinazowazunguka kwa kushirikiana na wadau mbali mbali,
·        Uboreshaji wa huduma za uibuaji wa wagonjwa kupitia ushirikishwaji wa vitengo vyote katika vituo vya kutolea huduma za afya,
·        Kushirikisha jamii katika kuibua wahisiwa wa Kifua kikuu na Ukoma na kuwapeleka kwenye vituo vya kutolea huduma za afya kwa uchunguzi na tiba
·        Kuimarisha mikakati ya uibuaji watoto wenye maambukizi ya Kifua kikuu na kuanzisha dawa mpya za Kifua kikuu kwa watoto,
·        Kugatua huduma za Kifua kikuu sugu kwa kushirikisha vituo vingine zaidi ya Hospitali ya Magonjwa ya Kuambukiza ya  Kibong’oto na kuanzisha  matibabu ya muda mfupi ya Kifua kikuu sugu kutoka miezi 24 hadi miezi 9,
·        Kuimarisha mfumo wa ukusanyaji wa taarifa za Mpango kwa mfumo wa kielektroniki.
Kwa upande wa ugonjwa wa Ukoma, ni wazi kuwa, ukubwa wa tatizo la ugonjwa huo linapungua kila mwaka na waathirika wengi bado tunawapata wakiwa tayari wamepata ulemavu. Kuna watanzania wenzetu takribani 300 kila mwaka hupata ulemavu wa kudumu utokanao na ukoma; ulemavu huu unazuilika kabisa. Takwimu za Mpango za mwaka 2015 zinaainisha kuwa wilaya ambazo bado zina wagonjwa wengi wa ukoma ni Masasi, Nanyumbu, Namtumbo, Liwale, Ruangwa, Mkinga, Kilombero, Chato na Nkasi.  Hivyo basi ni jukumu letu sote kuongeza juhudi za kupambana na Ukoma kwa kuongeza ubunifu katika kutafuta njia na mbinu mpya za kuhakikisha wagonjwa wanagunduliwa mapema na kupatiwa matibabu kwa wakati.  
Miongoni mwa mafanikio yaliyopatikana katika kudhibiti Ukoma nchini ni pamoja na:
·        Asilimia 95 ya wenye Ukoma hafifu na asilimia 93 ya wenye ukoma mkali walioanzishiwa matibabu walipona kabisa

Ndugu Waratibu,
Nitoe rai kwa mikoa na wilaya kushirikisha wadau wote katika kutekeleza mikakati iliyoainishwa na Mpango ambayo inalenga kutimiza malengo ya kitaifa ya kudhibiti Kifua kikuu kitaifa na kidunia. 
Ni matumaini yangu kwamba mkutano huu utakuwa ni chachu ya kuibua changamoto tulizo nazo, kujifunza kutoka kwa kila mmoja wetu na hivyo basi kuweza kuimarisha mipango na mikakati yetu ili tuwapatie wananchi huduma bora na endelevu. Ni jukumu la kila mmoja wetu kuhakikisha wagonjwa wenye Kifua kikuu na ukoma wanaibuliwa na kupatiwa matibabu kwa wakati. Kila mtumishi atimize wajibu wake.
Napenda kusisitiza na kuwaasa juu ya utekelezaji bora wa kazi za Mpango na matumizi sahihi ya fedha zinazofadhiliwa na wadau wetu wa maendeleo na kuzitolea taarifa kwa wakati ili kuendana na kasi ya Serikali ya awamu ya tano, yaani “HAPA KAZI TU



Ndugu Waratibu,
Serikali inapenda kuchukua fursa hii kuwashukuru wadau wa maendeleo kama vile Global Fund ATM, Shirika la Afya Duniani (WHO) Serikali ya Marekani kupitia USAID na mashirika yanayotekeleza shughuli za Kifua kikuu nchini kwa juhudi zao za kuisaidia serikali katika kupambana na magonjwa haya. Mchango wenu ni muhimu sana katika kuhakikisha mikakati tuliyojiwekea inatekelezwa kwa ufanisi na  kwa wakati.

Ndugu washiriki, Mabibi na Mabwana
Nichukue fursa hii kutamka kuwa mkutano huu wa Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Kifua kikuu na Ukoma kwa mwaka 2017 umefunguliwa rasmi.
Mungu ibariki Africa Mungu ibariki Tanzania Asanteni kwa kunisikiliza.

TAHADHARI YA MATAPELI




AMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO
  

TAARIFA KWA UMMA
TAHADHARI YA MATAPELI

Wizara ya Afya,Maendeleo ya Jamii, Jinsia,Wazee na Watoto inapenda kuutahadharisha Umma dhidi ya matapeli wanaopita maeneo mbali mbali wakiwaeleza watu kwamba wanauwezo wa kuwapatia Ajira za Afya, huku wakiwataka kutoa rushwa, kitu ambacho si kweli na ni kinyume na sheria na taratibu za nchi. Katika watu hao kuna mtu anayetumia jina la Godfrey Nyami  anaejifanya ni mtumishi wa Idara ya Utawala Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto na huchukua fedha kiasi cha shilingi 100,000/ kwa ahadi ya kuwapatia kazi.
Kama kuna mtu yoyote anafanya hivyo na unamfahamu tafadhari  toa taarifa katika vyombo vya dola, kwani kufanya hivyo ni kosa kisheria na hatua kali zitachukuliwa.

Imetolewa na ,

Kitengo cha Mawasiliano Serikalini-Afya
27/11/2017.

Jumamosi, 25 Novemba 2017

SERIKALI YATARAJIA KUTOA RESENI KWA HOSPITALI NA VITUO VYA AFYA VYA UMMA VITAKAVYOKIDHI VIGEZO VYA UBORA.

 Dkt.Ndugulile akimkabidhi Kaimu Mganga Mkuu wa Wilaya ya Nanyumbu Dkt.Furaha Mwakafyila Ngao baada ya kuibuka mshindi wa Huduma za afya katika vituo vya afya.

 Afisa Tawala wa Wilaya ya Nanyumbu Salumu Palango akimpongeza Kaimu Mganga Mkuu wake baada ya kupokea ngao.

 Mkurugenzi wa Idara ya Ubora na Uhakiki wa Huduma za Afya toka Wizara ya Afya Dkt.Mohamed Mohamed akielezea tathimini ilivyofanyika katika Mkoa huo mwaka 2016 na Halmashauri ya Wilaya ya Nanyumbu Kuibuka mshindi kwa kupata ngao na cheti.

 Mkuu wa Wilaya MHE.Evod Mmanda akiongea wakati wa mkutano huo.

 Naibu Waziri Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto Dkt.Faustine Ndugulile(katikati)akiongea na Viongozi na Watendaji wa Afya Afya Mkoa na Wilaya ya Mtwara wakati wa zoezi la kutoa ngao na vyeti kwa  vituo vya afya vilivyo na ubora wa huduma za afya.Kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Mtwara Mhe.Evod Mmanda na kulia ni Mganga Mkuu wa Mkoa Dkt.Wedson Sichalwe.

 Naibu Waziri akimpongeza Kaimu Mganga Mkuu wa Wilaya ya Nanyumbu baada ya kuibuka mshindi.Dkt.Ndugulile aliipongeza Wilaya hiyo kwa mpangilio mzuri wa utoaji huduma pamoja na utunzaji wa kumbukumbu kwenye stoo ya dawa katika kituo cha afya cha Mtambaswala ambacho kimeanza miezi miwili iliyopita lakini kimeonyesha ufanisi wa hali ya juu.

 Picha ya pamoja mara baada ya Naibu Waziri kutoa ngao na vyeti kwa washindi kwa Mkoa wa Mtwara.

 Dkt.Ndugulile akisoma taarifa ya dawa katika Zahanati ya Ziwani iliyopo Manispaa ya Mtwara,ambapo Naibu Waziri huyo alichukizwa hali ya miundombinu na uwajibikaji wa Zahanati hiyo na kuwapa miezi miwili wawe wamefanya marekebisho kama walivyoelekezwa.






Na.WAMJW,Mtwara

Serikali inatarajia kutoa leseni kwa hospitali na vituo vya afya vya Umma vitakavyokidhi vigezo vya ubora wa kutoa huduma za afya ili mwananchi  wajue kituo atakachoenda kina ubora gani wa huduma hivyo nchini

Hayo yamesemwa jana na Naibu Waziri wa Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto Dkt.Faustine Ndugulile wakati akiongea na Viongozi na Watendaji wa afya wa Mkoa na Wilaya zake kwenye ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mtwara wakati wa zoezi la kutoa ngao kwa wilaya iliyofanya vizuri na vituo vya afya vilivyofanya vizuri wakati wa zoezi la tathimini ya kutoa nyota kwa vituo vya kutolea huduma za afya.

Dkt.Ndugulile alisema hivi sasa serikali inasisitiza kuweka ubora wa huduma za afya  katika vituo vyote vya afya vya umma ili kukidhi ubora unaotakiwa wa kutoa huduma kwa wananchi”tunakwenda mbali zaidi  usipokuwa na vigezo hospitali yako na kituo chako  hutopewa leseni”

Hata hivyo amewataka wale wote waliopewa maelekezo ya nini wafanye basi viongozi wawajibike kwa kurekebisha changamoto zilizopo na wasingoje idara ya uhakiki ubora  kutoka wizarani waje kukagua kwani Lengo liliowekwa na wizara ni kila kituo cha afya kupata nyota tatu  hadi kufikia mwezi juni mwakani.

“Nyinyi wengine wote hamkustahili kupata cheti hata kimoja hapa,Mkoa wa Mtwara asilimia 3 za vituo vyenu vina nyota mbili na asilimia  51 vina nyota moja na zaidi ya nusu mna nyota 1 na asilimia 46 mna nyota sifuri hali ya utoa huduma bado”Nimetoka hapo zahanati ya Ziwani,kwakweli hapana,ubora wa kutoa huduma pale hapana wakati mpo mjini.

Kwa upande mwingine amewataka kamati za afya ngazi ya Mkoa na Wilaya kufanya kazi na kusimamia katika kuyafanyia kazi maelekezo yote waliyopatiwa kwani maboresho mengine hayahitaji fedha hivyo kamati hizo zitimize wajibu wao”Niwaombe mbadilike kwani mambo madogo madogo yatakuja kuwagharimu hivyo msimamie hali ya utoaji wa ubora na huduma za afya kwa mkoa wa mtwara ni mbaya,nikirudi wakati mwingine sitoongea kirafiki hivi”alisisitiza

Aidha,aliwataka watendaji hao kubadilika katika utendaji wao na hivyo kusimamia upatikanaji wa dawa katika vituo vyao vya afya ili kusiwepo na malalamiko kutoka kwa wananchi kwamba wamekosa dawa
“Dhama imebadilika,hivyo kila mmoja awajibike,awamu hii ni nyingine,hatutaki kusikia dawa hakuna na mwananchi analalamika amekosa dawa kwenye kituo cha afya,Mhe.Rais anaipenda sekta ya afya na ameongeza bajeti ya dawa na anatoa pesa zote,sitaki kusikia dawa hakuna na Wilaya itakayoshindwa basi viongozi wake nao hawatoshi”aliongeza Naibu Waziri

Naye Mkurugenzi wa Idara ya Uhakiki Ubora  toka Wizara ya afya Dkt. Mohamed Mohamed alisema wizara ilingia kwenye mpango wa kuboresha huduma kwenye vituo vinavyotoa huduma za afya ya Msingi mwaka 2014 kwa kuhusisha kufanya tathimini vituo vyote vya afya nchini na kuvipa kategoria ya nyota  moja hadi tano ikiwemo wa kuandaa mipango ya kuimarisha ubora katika vituo hivyo.
"Tathimini ya awali ilifanyika katika vituo vyote vya kutolea huduma za afya ya msingi nchini mwaka Aprili,2015 na Desemba 2016"

Alitaja maeneo yaliyoangaliwa na kufanyiwa tathimini ni uendeshaji wa vituo ,utendaji wa wafanyakazi,uwajibikaji,miundombinu ya kituo,mkataba kwa mteja pamoja na mazingira salama ya kutolea huduma na ubora wa huduma wenyewe.
Jumla ya vituo 6997 vilifanyiwa tathimini nchini na katika Mkoa wa Mtwara tathimini ya awali ilifanyika mwezi mei 2016 na vituo 221 vilifanyiwa tathimini na matokeo ya awali yalikua vituo 6 vilipata nyota 2(3%),vituo 112 vilipata nyota 1(51%) na vituo 103 vilipata nyota 0(47%).

Katika zoezi hilo Halmashauri ya Wilaya ya  Nanyumbu iliibuka mshindi kwa kupata ngao,na kituo cha afya Nanyumbu kilipata cheti.Kituo kingine cha afya kilichopaya cheti ni kituo cha Nagaga cha Masasi pamoja na za zahanati ya Nanjota na Nambaya zote za Halmashauri ya Masasi zilifanya vizuri.Pia zahanati ya Shangani ya halmashauri ya Manispaa ya Mtwara ilipata cheti.

Ijumaa, 24 Novemba 2017

UPASUAJI WA KIHISTORIA WA UPANDIKIZAJI WA FIGO WAFANYIKA.

- Hakuna maoni
 Waziri wa Afya, Maendeleo ya jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu akisisitiza jambo mbele ya jopo la madaktari bingwa wa Upasuaji wa upandikizaji wa figo kutoka Tanzania na India pamoja na Waandishi wa habari (hawapo kwenye picha), katika uzinduzi rasmi wa huduma za upasuaji wa upandikizaji wa figo uliofanyika katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.

 
 Madaktari  Bingwa kutoka Hospitali ya Taifa ya Muhimbili  walioshiriki katika Upasuaji wa upandikizaji wa figo kwa kushirikiana na Jopo la madaktari bingwa kutoka Hospitali ya BLK ya New Delhi, India.

 Prof. Lawrence Museru akimueleza jambo Waziri wa Afya, Maendeleo ya jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu wakati wa uzinduzi rasmi wa huduma za upasuaji wa upandikizaji wa figo uliofanyika katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili .

 Mkuu wa Kitengo cha Upandikizaji wa Figo kutoka India Dkt. H.S Bhatyal akimtambulisha Mkurugenzi Mkuu wa Nephroway Dkt. Sunil Prakash  mbele ya  Waziri wa Afya, Maendeleo ya jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu.

Picha ya pamoja ikiongozwa na Waziri wa Afya, Maendeleo ya jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu katika uzinduzi rasmi wa huduma za upasuaji wa upandikizaji wa figo uliofanyika katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.




Na WAMJWW, DSM
Hospitali ya Taifa ya Muhimbili ikishirikiana na wataalam kutoka Hospitali ya BLK ya New Delhi, India, wamefanikiwa kufanya upasuaji wa kihistoria wa upandikizaji wa figo (Renal Transplant).
Hayo yamesemwa na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu wakati wa uzinduzi rasmi wa upandikizaji wa figo uliofanyika katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili jijini Dar es salaam.
“Kupitia hadhara hii nipende kutumia fursa hii kuwafahamisha rasmi Watanzania kwamba sasaivi Hospitali yetu ya Taifa ya Muhimbili kwa kushirikiana na Hospitali ya BLK ya New Delhi, nchini India wamefanikiwa kufanya upasuaji wa upandikizaji wa figo” alisema Mh. Ummy
Pia Waziri Ummy amesema kuwa kuanzishwa kwa huduma hizi zakibingwa za kupandikiza figo hapa nchini ambazo awali zilikua hazipatikani kutaleta nafuu katika gharama ambazo zingetumika, hii inatokana na ongezeko kubwa la wagonjwa wa figo huku wengi wao wakihitaji huduma ya utakasishaji damu (Renal Dialysis).
Kwa upande mwingine Mh. Ummy ameongeza kuwa Serikali imeanzisha vituo vya utakasishaji damu katika hospitali za Mbeya Rufaa, Chuo Kikuu cha Dodoma, KCMC na Bugando kwaajili ya  wagonjwa wanaohitaji huduma za dialysis. Vile vile, huduma hii inapatikana katika hospitali za binafsi hapa Dar es Salaam zikiwemo za Kairuki, TMJ, Regency, Aga Khan, Access na Hindu Mandal.
Mh. Ummy  Mwalimu amewahasa Watanzania kuendelea kuiamini Hospitali ya taifa ya Muhimbili kutokana na huduma bora zinazotolewa na amewahakikishia serikali itaendelea kuboresha huduma zaidi katika vituo vyote vya Afya nchini.
Aidha Mh. Ummy Mwalimu (MB) ameendelea kuwakumbusha na kuwahasa Watanzia kujiunga na mifuko ya Bima ya Afya ili kupunguza gharama kubwa inayoweza kuwakumba pindi watakapopata magonjwa.
Pia Mh. Ummy (MB) hakusita kumpongeza Raisi wa awamu ya Tano Dkt. John Pombe Magufuli kwa kwa kuwa karibu sana na sekta ya Afya kwa  kuboresha huduma za matibabu yakibingwa,
“Wakati Mh. Raisi anaingia madarakani Muhimbili walikuwa wana vitanda vya ICU 21 tu, leo Muhimbili wanavitanda 74, wagonjwa 74 wanaweza kuhudumiwa mara moja kwa wakati mmoja ambao wanahitaji huduma za dharura” alisema Mh. Ummy Mwalimu.
Nae Mkurugenzi Mkuu wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili Prof. Lawrence Museru amewashukuru Madaktari bingwa wa upandikizaji wa figo kutoka Hospitali ya BLK ya New Delhi India kwa kukubali kutoa mafunzo kwa madaktari wa Tanzania bila gharama yoyote.


SERIKALI KUTOA MUONGOZO WA UTOAJI TIBA KWA HOSPITALI ZOTE

- Hakuna maoni


Na.WAMJW,Ruangwa
Wizara ya Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na watoto inatarajia kutoa mwongozo wa utoaji tiba kwenye hospitali zote nchini ili kuwe na mfumo mzuri wa  dawa muhimu ili kuepusha madaktari kuagiza dawa ambazo zipo nje ya mfumo wa dawa muhimu.
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Afya Dkt.Faustine Ndugulile wakati wa ziara yake ya kuangalia hali ya upatikanaji wa dawa kwenye vituo vya kutolea huduma za afya vya Serikali 
“Kabla ya mwisho wa mwaka tunataka kutoa muongozo huo(Standard  Treatment Guidline) kwa sababu imekua changamoto kwani wale wauzaji wakubwa  wa dawa wamekua wakizitembelea hospitali kubwa na kuwarubuni  wanunue dawa zao ambazo zipo nje ya dawa zetu muhimu”
Kwahiyo muongozo huo itakua kila ugonjwa dawa ya kwanza itakua ipi na kama itashindika dawa itakayofuata dawa ipo na hizo dawa zitaagizwa na kutunzwa na  Bohari ya Dawa(MSD)
Hata hivyo Dkt.Ndugulile amewataka watendaji wa hospitali hiyo kuweka utaratibu na mpangilio  mzuri na unaohitajikwa  wa utunzaji wa dawa kwenye stoo ya madawa iliyopo hospitalini hapo,baada ya kukuta hakuna upangaji mzuri wa dawa na vifaa tiba
“mmenithibitishia kwamba dawa zote mnazipata kwa asilimia 90 hivyo ni vyema Mfamasia wa Wilaya kuzipanga dawa hizo vizuri na kuweka kiyoyozi ambacho kitasaidia kutunza dawa kwa muda bila kuharibika”
Alisema  hivi sasa nchi haina tatizo la upatikanaji wa dawa kwani bajeti ya dawa hivi sasa imeongezeka kutoka  shilingi bilioni 30  mpaka zaidi ya bilioni 260 kwa mwaka huu wa fedha “bajeti hii imekua ikitolewa na Mhe.Rais amekua akizitoa fedha zote,hivyo hatuna shida ya fedha hivyo nasi hatutarajii kuwa na shida ya dawa na dawa tunazokuwa tunazipata zitunzwe vizuri”
Aidha,amezitaka kamati za afya katika ngazi za zahanati,vituo vya afya na hospitali zinafanya kazi ipasavyo kwa kusimamia matumizi mazuri ya dawa
Kwa upande wa ubora wa huduma za afya kwa vituo vya kutolea huduma za afya vya serikali hivyo kumekua na mkakati wa kuwa na ubora wa vituo vya serikali kwa kuwapatia nyota kulingana na ubora uliopo kwenye vituo kwa kuangalia utoaji wa huduma,maabara na sehemu zingine za kutolea huduma
Kwa upande wa Mfuko wa afya wa jamii(CHF) Dkt.Ndugulile amewapongeza wilaya hiyo kwa kusajili  kaya 13,788 kutoka 978 mwaka 2016/2017,ambapo wamewapatia vitambulishovya matibabu wazee 4,000.
“hivi sasa Serikali inataka kuwa na bima kwa wote kwani gharama ya matibabu kwa sasa ni kubwa sana  hasa na kumekua na ongezeko la  magonjwa yasiyo ya kuambukizwa,hivyo tunataka kuwasaidia wananchi ambao hawawezi kumudu gharama hizo ili anavyokwenda kwenye vituo vyetu asiwaze masuala ya kutoa fedha”alisema Dkt.Ndugulile.
Akisoma ripoti ya Wilaya hiyo Kaimu Mganga Mkuu wa Wilaya hiyo Dkt.   Ernest Ntahuka Alisema Halmashauri hiyo imeweza kuboresha hali ya upatikanaji wa dawa kwa asilimia 85 kutoka asilimia 60 ya mwaka 2015/2016
Hata hivyo alisema Halmshauri ya Ruangwa kwa mwaka 2017/2017 imetenga shilingi milioni 650 kwa ajili ya ujenzi wa hospitali mpya ya wilaya na tayari imeshatenga eneo la ujenzi lenye ukubwa wa hekari 60 ambapo ramani ya ujenzi huo tayari imeandaliwa


Alhamisi, 23 Novemba 2017

LINDI WATAKIWA KUSHIRIKI KATIKA ZOEZI LA UMEZAJI KINGATIBA YA MAGONJWA YALIYOKUWA HAYAPEWI KIPAUMBELE, ASEMA DKT. FAUSTINE NDUGULILE

Naibu Waziri wa Afya Dkt.Faustine Ndugulile akikata utepe kuashiria uzinduzi wa upasuaji wa mabusha na ngirikokoto kwa wagonjwa wapatao 200 wa Manispaa ya Lindi. Kulia kwake ni Mkurugenzi wa Statoil Bw.Oyotein Michelsen na kushoto kwake ni Mkurugenzi wa Kinga toka Wizara ya Afya Dkt.Neema Rusibamayila.

  Naibu Waziri wa Afya Dkt.Faustine Ndugulile akimjulia hali mmoja ya wagojwa wakati wa ziara yake katika hospitali ya rufaa ya Mkoa Sokoine mkoani Lindi. pembeni yake ni Mkurugenzi wa Statoil Bw.Oyotein Michelsen.

  Mkurugenzi wa Statoil Bw.Oyotein Michelsen akisoma hotuba kwenye ufunguzi wa kambi ya upasuaji inayofanyila kwenye hospitali ya rufaa ya Mkoa Sokoine mkoani Lindi

 Baadhi ya wananchi wanaotarajia kufanyiwa upasuaji wa magonjwa hayo.

 Naibu Waziri wa Afya akimkabidhi Mkurugenzi wa Kinga toka Wizara ya Afya Dkt.Neema Rusibamayila ambapo Mpango wa Taifa wa kutokomeza Magonjwa yaliyokuwa hayapewi Kipaumbele ndiye mratibu wa upasuaji huo.

 Dkt.Faustine Ndugulile akipokea mashine ambayo ina kisu cha moto ambacho kinazuia damu wakati wa upasuaji kutoka kwa Mkurugenzi wa Statoil.

 Dkt.Faustine Ndugulile akihutubia wananchi waliofika kwenye uzinduzi wa upasuaji wa mabusha na ngirikokoto kwa wagonjwa wapatao 200 wa Manispaa ya Lindi.

Naibu Waziri wa Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto akipokea hundi yenye thamani ya shilingi milioni 264 toka kwa Mkurugenzi wa Kampuni ya utafiti na uchimbaji wa mafuta ya Statoil bw.Oyotein Michelsen .Fedha hizo ni kwa ajili ya kambi za upasuaji wa mabusha na ngirikokoto kwa watu wapatao 400 kwa mwaka 2017 na 2018.





Na WAMJW-LINDI

WAKAZI wa Lindi na vitongoji vyake wametakiwa kushiriki katika kampeni ya kutokomeza magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele kwa kumeza kingatiba za kutokomeza magonjwa hayo pamoja na kutunza mazingira kwa kuondoa mazalia ya mbu wanaenezao magonjwa hayo.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile wakati wa uzinduzi wa kambi ya upasuaji wa Mabusha na Ngirikokoto(Henia) unaofanyika mkoani Lindi.

"Wakazi wa Lindi na Vitongoji vyake tunatakiwa kushiriki katika zoezi la kumeza dawa za kukinga  magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele pamoja na kufanya usafi wa mazingira ili kuondoa mazalia ya mbu"alisema Dkt. Ndugulile

Aidha, Dkt. Ndugulile amewataka wananchi wa Lindi  kuondoa dhana potofu ya kuwa kila mwenye mabusha au ngirimaji basi atakuwa amerogwa ila ajue ugonjwa huo unasababishwa na vimelea vinavyotokana na mbu na kuzingatia umezaji wa dawa hizo.

Dkt. Ndugulile amesema kuwa katika kuhakikisha wanapambana kutokomeza ugonjwa huo Serikali kwa kushirikiana na Kampuni ya Utafiti ya uchimbani mafuta na gesi ya Statoil wamepata fedha za kuwafanyia upasuaji wagonjwa 200 wa mabusha na ngirikokoto kwa awamu ya kwanza ya mwaka 2017 na wagonjwa 200 kwa awamu ya pili ya mwaka 2018.

Mbali na hayo Dkt. Ndugulile amesema kuwa wananchi wa Lindi wanatakiwa kutoa taarifa sehemu husika pindi wanapoambiwa kuwa dawa muhimu hakuna kwenye vituo vya afya vya Serikali kwani dawa hizo zipo kwa asilimia 90 Mkoani humo.

Kwa upande wake   Katibu Tawala wa Mkoa wa Lindi Bw. Ramadhani Kaswa amesema kuwa umezajii wa kingatiba ya magonjwa hayo umefikia asilimia 70 kwa mwaka 2016/2017.

Aidha, Bw. Kaswa amesema kuwa kutokana na zoezi la kuwatambua wagonjwa wenye mabusha na ngirikokoto wamejiandikisha wagonjwa 1294 kwa mkoa wa Lindi ikiwemo Manispaa ya Lindi wagonjwa 67,Wilaya ya Nachingwea wagonjwa 101,Halmashauri ya Lindi wagonjwa 633, Wilaya ya Liwale wagonjwa 387 na Wilaya ya Luongo wagonjwa 106.

Uzinduzi huo uliambatana na zoezi la kumeza Kingatiba za  magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele ikiwemo mabusha na matende,usubi,minyoo,trakoma(vikope) na vichocho.

Jumatano, 22 Novemba 2017

WACHIMBAJI WADODO WADOGO WA MADINI WAPATA AHUENI KWENYE AFYA

 Waziri wa Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto Ummy Mwalimu akisaini kitabu cha wageni mara baada ya kufika kwenye hospitali ya Magonjwa ya kuambukiza Kibong'oto Mkoani Kilimanjaro,kushoto ni Mkuu wa Mkoa huo Mhe.Anna Mghirwa

 Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Mhe.Anna mghirwa akiongea  wakati wa ufunguzi wa kiyuo hicho ambacho kitakuwa kikihudumia wachimbaji wa madini na familia zao kutokana na kifua kikuu na kudhurika na magonjwa ya mfumo wa hewa.

 Baadhi ya wachimbaji wa madini kutoka Mererani ambao walishiriki ufunguzi wa kituo hicho

 Baadhi ya watumishi wa Hospitali ya Kibong'oto wakimsikiliza Waziri Ummy Mwalimu(hayupo pichani)wakati akihutubi ambapo alisema kituo hicho ni miongoni mwa vituo 11 vilivyojengwa katika nchi 10 za SADC

 Waziri wa Afya pamoja na viongozi wa Mkoa,Mbunge pamoja na wadau wa madini wakikata utepe kuashiria ufunguzi wa kituo hicho.

 Waziri Ummy Mwalimu(wa kwanza kushoto),Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Mhe.Anna Mghirwa(kulia) walikagua chumba chenye mashine ya Uchunguzi (Xray) iliyofungwa kwenye kituo hicho.

Waziri wa Afya (katikati)akimsikiliza kwa makini bw.Athumani Abdalah(hayupo pichani)wakati akitoa ushuhuda wake kama mchimbaji mdogo mdogo,kishoto ni Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Mhe.Anna Mghirwa na kulia kwake ni Mbunge wa Jimbo la Siha Dkt.Godwin Mollel



Na.WAMJW,Siha

Shughuli za uchimbaji madini duniani kote zinatambulika kama ni shughuli hatarishi kwa afya ya binadamu kutokana na urahisi wa kudhurika pia athari kwenye afya ya mapafu kutokana na vumbi zito

Hayo yamesemwa na jana na Waziri wa Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto Ummy Mwalimu wakati wa ufunguzi wa kituo cha kisasa cha kutoa huduma za Kifua Kikuu,UKIMWI na Magonwa yatokanayo na shughuli za uchimbaji madini katika hospitali ya magonjwa ya kuambukiza Kibong'oto iliyopo Mkoani Kilimanjaro

Waziri Ummy amesema shughuli za uchimbaji humuweka mchimbaji kwenye hatari zaidi ya kupata kwa urahisi ugonjwa wa Kifua Kikuu na Magonjwa mengine sugu ya mfumo wa njia ya hewa,vile vile shughuli za kijamii,kiuchumi na kiutamaduni katika maeneo ya migodi zimekua zikichochea kasi ya maambukizi ya Ukimwi katika maeneo hayo.

"Kutokana na changamoto hizi na ili tupunguze tatizo LA Kifua Kikuu na UKIMWI katika sekta ya madini,mwaka 2015 nchi kumi za SADC kwa pamoja ziliomba fedha katika mfuko wa Dunia wa Kudhibiti magonjwa ya UKIMWI,Kifua Kikuu na Malaria(Global fund ATM) ili kukabiliana na tatizo hili katika sekta ya madini"(TB in the Mining Sector(TIMS)

Aidha,alisema tangu kuanza kutekelezwa kwa mradi huo Januari,2016,tayari matokeo ya utafiti zilizofanyika maeneo ya migodi yameonesha kuwepo kwa kiwango kidogo cha ufahamu na uelewa wa masuala ya Kifua Kikuu,UKIMWI na magonjwa yatokanayo na shughuli za uchimbaji miongoni kwa wachimbaji na jamii inayowazunguka.

" wachimbaji wadogo wadogo wameendelea kuathirikanna vumbi LA silika kutokana na kutumia dhana duni za uchimbaji usiozingatia masharti ya udhibiti wa vumbi,licha ya sekta hii kuchangia kwa kiasi kikubwa pato LA Taifa,hali a upatikanaji wa huduma za afya kwenye migodi si ya kuridhisha"

Kituo hicho cha kisasa ambacho ni cha kwanza nchini kitakua mfano na kitasaidia kuokoa maisha na ulemavu utokanao na shughuli za uchimbaji kutokana sehemu zingine nchini,kimefungwa vifaa vya uchunguzi ikiwepo xray na kupatiwa daktari bingwa na wataalamu wa maabara na mionzi

Jumanne, 21 Novemba 2017

KIKAO KAZI CHA KUJADILI UTEKELEZAJI WA MIKAKATI, SERA NA MIONGOZO YA TEHAMA KATIKA SEKTA YA AFYA CHAENDELEA JIJINI NDODOMA.

- Hakuna maoni
Mwakilishi wa Katibu Mkuu, Mkurugenzi wa sera na mipango,, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto , akiwa katika picha ya pamoja na Maafisa TEHAMA kutoka Wizara ya Afya na Taasisi zake.

  Mkuu wa kitengo cha TEHAMA, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, ndugu Hermes S. Rulagirwa, akiwakaribisha  Maafisa TEHAMA kutoka Wizara ya Afya na Taasisi zake.

 Mwakilishi wa Katibu Mkuu, Mkurugenzi wa sera na mipango, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto (WAMJW),Ndg Edeard Mbanga Akifungua kikao cha maafisa TEHAMA wa Wizara na Taasisi zake, kinachopitia utekelezaji wa mpango mkakati wa eHealth Strategy 2013-2018. Kikao hiki kinafanyika katika ukumbi wa LAPF Dodoma.





Na WAMJWW
 
Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto leo imeendelea na utekelezaji wa mkakati wa matumizi ya TEHAMA katika Sekta ya Afya (Health Strategy 2013-2018) katika ukumbi wa LAPF jijini Dodoma. 
Sambamba na hiyo, Wizara kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais TAMISEMI, Wakala ya Serikali Mtandao (EGA), imetoa mwongozo unaoelekeza namna bora ya usimikaji na matumizi ya mifumo ya kielektroniki katika sekta ya Afya.
Malengo ya kikao kazi hiki ni kuwajengea ufahamu wa pamoja washiriki juu ya mikakati, sera na miongozo ya TEHAMA iliyopo katika sekta ya Afya. Vilevile, kupata maendeleo ya mikakati yote ya TEHAMA kutoka katika Miradi, Taasisi na Hospitali zote zilizopo chini ya Wizara. 
Hata hivyo, kikao kazi hiki kinajadili kwa upana mafanikio na changamoto ya utekelezaji wa mkakati huu wa 2013-2018 ili  kuboresha mkakati mpya wa mwaka 2018-2023.

Jumatatu, 20 Novemba 2017

WAZIRI UMMY AWATAKA WAGANGA WAKUU WA MIKOA KUANZISHA ZOEZI LA WAZI UCHUNGUZI WA SARATANI YA KIZAZI KWA WANAWAKE.

 Waziri  Wa Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu akiongea na waandishi wa habari hawapo pichani wakati wa kupokea vifaa vya kuchunguza saratani vyenye thamani ya shilingi milioni 98  leo jijini Dar es salaam.

 Waziri  Wa Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu kulia akipokea moja ya vifaa vya uchunguzi wa saratani ya kizazi kutoka kwa Mkurugenzi Mkazi wa Jhpiego nchini Tanzania Bw. Jeremia Zoungran kushoto wakati wa makabidhiano ya vifaa vya kuchunguza saratani ya kizazi leo jijini Dar es salaam.

 Waziri  Wa Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu kulia akipokea moja ya nyenzo za  kufundishia juu ya uchunguzi wa saratani ya kizazi kutoka kwa Mkurugenzi Mkazi wa Jhpiego nchini Tanzania Bw. Jeremia Zoungran kushoto wakati wa makabidhiano ya vifaa vya kuchunguza saratani ya kizazi leo jijini Dar es salaam katikati ni Afisa Afya kutoka USAID Bi. Ananth Thambinyga.

 Mkurugenzi Mkazi wa Jhpiego nchini Tanzania Bw. Jeremia Zoungran akiongea na waandishi wa habari hawapo pichani wakati wa kupokea vifaa vya kuchunguza saratani vyenye thamani ya shilingi milioni 98  leo jijini Dar es salaa.

Waziri  Wa Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu  katikati akiwa kwenye picha ya pamoja na baadhi ya watendaji wa  Wizara ya afya,Jhpiego na USAID wakati wa kupokea vifaa vya kuchunguza saratani vyenye thamani ya shilingi milioni 98  leo jijini Dar es salaam, wa tatu kushoto ni Mkurugenzi Mkazi wa Jhpiego nchini Tanzania Bw. Jeremia Zoungran na aliyevaa nguo ya pundamilia ni Afisa Afya kutoka USAID Bi. Ananth Thambinygan.



Na WAJWW-DSM
WAZIRI Wa Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu amewaelekeza waganga wakuu wa mikoa wote nchini kuanzisha zoezi la wazi la uchunguzi wa saratani ya kizazi angalau mara moja katika mwezi ili kusaidia kutokomeza tatizo kwa wanawake hilo nchini.
Hayo amesema wakati wa kupokea vifaa vya kuchunguza saratan vyenye thamani ya shilingi milioni 98  ambavyo vimetolewa na Taasisi isiyo ya Kiserikali ya JHPIEGO kwa kushirikiana na USAID ili kusaidia kupambana na tatizo hilo nchini.
“Angalau ifikapo Desemba 2018 nataka  vituo vya Afya vya Serikali  524  viwe vinatoa huduma ya matibabu ya awali ya Saratani ya mlango wa kizazi na kufikia  wanawake milioni 3 watakaopata huduma hii ili kuokoa wanawake wa vijijini  kwani mpaka sasa hivi tunavyo vituo vya afya  265 vinavyotoa huduma hii ” alisema Waziri Ummy.
Aidha Waziri Ummy amesema kuwa uchunguzi na kutoa chanjo ya Saratani ya mlango wa kikazi  kwa wasichana kuanzia miaka 9 mpaka 14 ili kuweza kupunguza vifo vitokanavyo na tatizo hilo kwani katika kila wanawake 100 vifo vinavyotokana na ugonjwa huo ni 32.
Mbali na hayo Waziri Ummy amesema kuwa katika kuongeza jitihada za  kupambana na ugonjwa huo Serikali imeongeza vituo vya afya 100 kutoka 343  hadi kufikia 443 mwaka huu ili kutokomeza tatizo hilo nchini.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkazi wa Jhpiego nchini Tanzania Bw. Jeremia Zoungran amesema kuwa walianzisha mpango wa kupambana na tatizo hilo na kufanikiwa kuwafikia wanawake elfu 75 kwa mikoa 4 tangu mwaka 2009.
“Mbali na mikoa hiyo 4 bado tunalengo la kuongeza mikoa mingine 7 ili kuweza kutoa huduma hiyo kwa ajili ya kuunga mkono Juhudi za Serikali katika kupambana na Saratani ya mlango wa kizazi ili kuweza kuokoa wanawake wengi zaidi nchini” alisema Bw. Zoungran.